1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakimbizi wa Rohingya wataka ulinzi wa Umoja wa Mataifa

Zainab Aziz
29 Aprili 2018

Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa umewatembelea wakimbizi wa Rohingya nchini Bangladesh na umeahidi kufanya kazi kwa bidii ili kutatua mgogoro wa wakimbizi hao.

https://p.dw.com/p/2wsGC
UN-Delegation besucht Rohingya-Flüchtlingscamp in Bangladesch
Picha: Getty Images/AFP/S. Jahan

Wakimbizi wa jamii ya Waislamu wa Rohingya wametoa mwito uliojaa hisia kwa ujumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa hii leo wakiomba wasaidiwe kurudi salama nchini Myanmar, lakini pia wakitaka haki kutendeka kutokana na sababu za kukimbia kwao nchini humo, ambazo ni mauaji, ubakaji na uchomaji wa makazi yao kwa makusudi. Kwenye ziara yao katika eneo lisilodhibitiwa na nchi yoyote miongoni mwa mataifa hayo jirani ya Myanmar na Bangladesh.

Baadhi ya wanawake na wasichana wakimbizi wa Rohingya
Baadhi ya wanawake na wasichana wakimbizi wa RohingyaPicha: Getty Images/AFP

Baadhi ya wanawake na wasichana walimlilia kwa uchungu balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa Karen Pierce, wakati walipomweleza madhila waliyoyapata. Maafisa wa Umoja wa Mataifa na makundi ya kutoa misaada yameeleza wasiwasi wao kwamba msimu wa mvua kubwa unaotarajiwa kuanza hivi karibuni utasababisha hali mbaya zaidi ya kiutu. Maelfu ya wakimbizi wanaishi kwenye kambi za muda zilizojengwa kwa miti ya mianzi na maturubai katika eneo la Kutupalong.  

Wanadiplomasia hao, walitembelea kambi za wakimbizi na maeneo ya mipaka ambako karibu Warohingya 700,000 wanaishi. Warohingya wanaoishi katika kambi za wakimbizi nchini Bangladesh wanadai ulinzi wa Umoja wa Mataifa wakati wa ziara hiyo ya wanadiplomasia wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika makazi ya wakimbizi ya kusini mashariki mwa Bangladesh.

Mwanadiplomasia Gustavo Adolfo Meza Cuadra Velasqez balozi wa Peru katika Umoja wa Mataifa anayeuongoza ujumbe huo wa watu 24 amesema ziara yao imetoa nafasi ya kushuhudia hali halisi. Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Dmitry Polyansky, amesema yeye na washiriki wenzake katika ujumbe huo hawatoupuuza mgogoro huo baada ya ziara yao hiyo, ingawa ameonya pia kuwa sio rahisi kupata suluhisho lake.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaotembelea kambi za wakimbizi wa Rohingya nchini Bangladesh
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaotembelea kambi za wakimbizi wa Rohingya nchini BangladeshPicha: Getty Images/AFP

Ujumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa umetembelea kambi inayowahifadhi maelfu ya wakimbizi wa jamii hiyo ya Waislamu wa Rohingya ili kusikiliza kilio cha wakimbizi hao. Maelfu ya wakimbizi walikusanyika katika kambi hiyo iliyoko Bangladesh kuukaribisha ujumbe huo.

Wakimbizi hao walibeba mabango, ambayo mengine yalisomeka "tunataka haki". Ujumbe huo ulikutana na baadhi ya wakimbizi 120 wakiwemo wahanga wa visa vya ubakaji na mateso. Ujumbe huo wa Umoja wa mataifa baada ya ziara yake ya siku tatu utaelekea Myanmar. Ujumbe wa wadiplomasia hao unawakilisha wajumbe kutoka nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama ambao ni China, Ufaransa, Urusi, Uingereza na Marekani pamoja na nchi 10 wanachama wasio wa kudumu.

UNHCR Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa
UNHCR Shirika la wakimbizi la Umoja wa MataifaPicha: DW/Shoib Tanha Shokran

Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa na Bangladesh hivi karibuni zilifikia mkataba wa maelewano kuhusu mchakato wa kuwarudisha nyumbani wakimbizi hao wa Rohingya. Mkataba huo unasisitiza kuwa ni lazima uwe salama na wa hiari na utakaozingatia heshima kulingana na viwango vya kimataifa. Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa Karen Pierce, amesema Baraza la Usalama litaendelea kufanya kazi ili kuwawezesha wakimbizi wanaorudi nchini Myanmar.

Warohingya wanakataliwa kupewa uraia nchini Myanmar, taifa lenye jamii kubwa ya Mabudha, ambapo jamii hiyo ya Waislamu wa Rohingya wamekabiliwa na mateso kwa miongo kadhaa. Wengi nchini Myanmar wanaamini kuwa Warohingya ni wahamiaji haramu kutoka Bangladesh. Idadi kubwa ya Warohinga wanaishi katika hali umaskini mkubwa katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar linalopakana na Bangladesh.

Mwandishi: Zainab Aziz/DPAE/APE

Mhariri: Lilian Mtono