1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpango wa Urusi na Uturuki kuvizima vita hivyo haupo tena

10 Juni 2019

Huenda zaidi ya wakimbizi milioni mbili wa machafuko nchini Syria wakakimbilia nchini Uturuki vita vitakapoendelea kupamba moto Kazkazini Magharibi mwa Syria huku fedha za misaada ya kiutu zikipungua kwa kiwango kikubwa

https://p.dw.com/p/3K8ds
Syrien Provinz Idlib Bewohner fliehen vor Kämpfen
Picha: Getty Images/AFP/A. Watad

Mshirikishi wa Umoja wa Mataifa katika mzozo wa Syria, Panos Moumtzis amesema wanahofia maelfu kwa mamilioni ya raia wa Syria watakimbialia katika mpaka wa Uturuki kutafuta hifadhi iwapo vita hivyo vitaendelea na kusababisha watu kuyakimbia makaazi yao. Akizungumza na shirika la habari la Reuters, Moumtzis amesema hali inaendelea kuwa mbaya na mpango wa Urusi na Uturuki wa kuvizima vita hivyo haupo tena.

Ameeleza kwamba mapigano hayo wameyaona yanalenga moja kwa moja ama kuathiri hospitali na shule katika sehemu za raia, hasa mijini kuliko na watu wengi, kitu ambacho hakifai kufanyika kulingana na sheria za haki za kibindamu ulimwenguni.

Jeshi la Syria linaloungwa mkono na Urusi limekuwa likiwashambulia waasi katika ngome yao ya mwisho kwa vita ya angani na ardhini jambo ambalo limelazimisha makumi kwa maelefu ya watu kuyakimbia makaazi yao. Mahsmabulizi hayo makali yalianza mwezi wa nne, yakiwa zaidi katika eneo la Kusini mwa mkoa wa Idlib na viunga vyake kama Hama na Latakia. Mashambulizi hayo ndio makali zaidi katika mgogoro baina ya rais Bashar Al-Assad na waasi.

Grenze Jordanien - Syrien | Rukban Flüchtlingslager 2017
Kliniki zinazoendeshwa na Umoja wa Mataifa karibu na kambi ya wakimbizi ya Rukban Picha: Getty Images/AFP/K. Mazraawi

Wahudumu wa mashirika ya kiutu wakosa uaminifu na wapiganaji

Mashirika ya usaidizi wa kiutu yamehimizwa kutambulisha sehemu waliko kwa pande zote mbili zinazozozana ili kuepuka kushambuliwa ila baada ya kuendelea kushambuliwa kwa hospitali kupitia mashambulizi ya angani wahudumu wengi wa mashirika ya kutoa usaidizi wa kiutu hawatoi taarifa kwa sababu ya kukosekana uaminifu upande wa wapiganaji.

"Kinachoendelea ni msiba mkubwa na miezi kadhaa iliyopita tulishauri vita hivyo visilenge maeneo ya watu na hospitali ila hilo sasa linafanyika mbele ya macho yetu wahudumu wa mashirika ya kiutu, hatua zinafaa kuchukuliwa kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu na wakimbizi wanaonusurika katika vita hivi," Moumtzis alisema.

Umoja wa Mataifa uliweka ombi la kutaka kupata dola bilioni 3.3 kushughulikia mahitaji ya kiutu nchini Syria mwaka huu ila licha ya ahadi nyingi kutolewa hadi sasa wamepokea dola milioni 500, jambo linalofanya usaidizi kuwa haba na usiotosheleze mahitaji.

(RTRE)