1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakristo washeherekea Krismasi

25 Desemba 2012

Wakristo duniani kote leo (25.12.2012) wanaadhimisha sikukuu ya Krismasi.

https://p.dw.com/p/178gC
Faithfuls attend an open air mass conducted by Pope Benedict XVI at Beirut City Centre Waterfront, September 16, 2012. REUTERS/Mohamed Azakir (LEBANON - Tags: RELIGION)
Papst Benedikt XVI in BeirutPicha: Reuters

Maelfu ya watu wamekusanyika katika mji wa Bethlehem kwenye Mamlaka ya Wapalestina kusheherekea sikukuu hiyo. Mji huo unaaminika kuwa ndiko pahala alikozaliwa masiha bwana yesu kristo.

Misa kubwa ilifanyika usiku wa kuamkia leo (25.12.2012) kwenye kanisa kongwe mjini humo na kuhudhuriwa na Rais Mahmoud Abbas. Padri Mkuu wa kanisa Katoliki kwenye eneo la Mashariki ya Kati, Fuad Twal ndiye aliyeongoza misa hiyo na kusema kuwa wanasheherekea si tu kuzaliwa kwa yesu kristo bali pia kuzaliwa kwa taifa la Palestina.

Katika kuadhimisha siku hii huko Rome ambako ndiko makao makuu ya Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Benedict wa 16 aliongoza misa kubwa usiku wa kuamkia leo.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedict wa 16

Ujumbe wa Baba Mtakatifu kwenye sikukuu hii ni kuwepo kwa amani kwenye eneo la mashariki ya kati. Amewataka pia watu wote duniani kumpa mungu nafasi kwenye maisha yao ya kila siku.

Baba Mtakatifu Benedict wa 16 akiongoza ibada
Baba Mtakatifu Benedict wa 16 akiongoza ibadaPicha: Reuters

Katika misa hiyo maalumu kwa ajili ya Krismas ambayo inawaunganisha Wakatoliki wapatao bilioni 1.2 duniani kote, Baba Mtakatifu ameonya pia kuhusu vitendo vya ubaguzi wa kidini.

Maelfu ya watu walimiminika katika viunga vya kanisa la Mtakatifu Peter mjini Vatican kwa ajili ya ibada hiyo ya takribani masaa mawili ambayo ilionyesha pia na vyombo vya habari mbalimbali duniani kote. Akiwa amshiba mslaba wake wa dhahabu na kuvalia mavazi yaliyopambwa kwa rangi ya dhahabu Baba Mtakatifu mwenye umri wa miaka 85 alionekana mwenye furaha.

Kiongozi huyo wa kanisa Katoliki duniani alisema " wacha tuombe mungu kwa ajili ya Waisraeli na Wapalestina ili waishi maisha ya amani ya mungu mmoja na uhuru". Ameiombea pia mizozo inayoendelea katika nchi za Syria, Lebanon, Iraq na majirani zao kwenye eneo la mashariki ya kati.

Baba Mtakatifu kutoa Baraka za Krismas

Aliomba akisema kuwa wakristu kwenye eneo hilo ambalo imani yao ilizaliwa wapate uwezo wa kuendelea kuishi huko, na kwamba wakristu na waislamu wajenge mataifa yao kwa ushirikiano kwa amani ya mungu.

Kijana wa Afrika Kusini akiuza mapambo ya Krismas
Kijana wa Afrika Kusini akiuza mapambo ya KrismasPicha: AP

Kiongozi huyo mzaliwa wa Ujerumani amepinga suala la kusema kuwa dini ndizo zinafaa kulaumiwa kwa machafuko yanayoendelea kwenye nchi mbalimbali duniani, ingawa alikubali kuwa dini inaweza baadhi ya wakati ikatumika vibaya. Akaonya " lazima tuwe waangalifu kwa maneno haya ya upotoshaji dhidi ya utukufu".

Hii leo kiongozi huyo atatoa baraka za siku hii majira ya mchana katika lugha mbalimbali kwa ajili ya miji na taifa. Wiki iliypita kiongozi huyo alipaza sauti kupinga ndoa za jinsia moja akisema mahusiano hayo yanakwenda kinyume na maumbile ya mwanadamu ambayo ni kuwepo baba. mama na watoto.

Krismas hii inakuja wakati kanisa katoliki likiwa limekumbwa na mkasa wa kuvuja kwa taarifa za ndani kwenye vyombo vya habari kuhusu masuala ya rushwa, mzozo wa madaraka.

Mwandishi: Stumai George/DPA/Reuters