1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakulima wazungu nchini Zimbabwe mashakani

Josephat Nyiro Charo30 Januari 2015

Wakulima wazungu wa Zimbabwe wanakabiliwa na vitisho vipya vya kufukuzwa kutoka mashamba yao. Wengi walipokonywa mashamba katika machafuko yaliyoanza mwaka 2000 na waliobakia sasa wameingiwa na wasiwasi.

https://p.dw.com/p/1ET4b
Simbabwe Tabakernte
Picha: AFP/Getty Images

Mandi Chimene, gavana mpya wa jimbo la Manicaland amesema katika mkutano wa hadhara mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba amewafukuza wakulima wazungu kutoka mashamba 12 katika wilaya ya Headlands pekee, akidai walikuwa wakilindwa na kundi la makamu wa rais wa zamani wa Zimbabwe, Joice Mujuru. Mujuru alitimuliwa kutoka chama tawala cha ZANU-PF mwezi Desemba mwaka uliopita baada ya kukosana na rais Robert Mugabe na mke wake, Grace Mugabe.

Grace ni miongoni mwa viongozi wa chama cha ZANU-PF wenye ushawishi mkubwa ambao wako mbioni kujinyakulia ardhi. Hivi majuzi polisi waliokuwa wakitimiza amri ya Grace Mugabe walivunja vibanda katika shamba la Manzou katika wilaya ya kilimo ya Mazowe, inayopatikana kiasi kilometa 40 kaskazini mwa mji mkuu, Harare. Mke huyo wa rais ambaye ana shamba lengine katika eneo hilo, alisema mwaka jana kwamba anataka kuligeuza shamba la Manzou kuwa mbuga ya wanyama itakayoleta fedha kwa ajili ya nyumba ya yatima.

Innocent Dube ni mmoja wa wakulima walioathiriwa katika zoezi hilo. Alisema, "Kama wanakuja usiku, hiyo ina maana wanatuogopa. Pengine hayo ni mateke ya mwisho ya farasi anayekaribia kufa, kwa sababu wameshindwa katika mahakama. Ina maana anajaribu kututisha tuondoke. Nimekasirika sana kwa sababu kila mara narudishwa nyuma. Ninapojaribu kujiimarisha naangushwa tena. Nitabaki pale nilipo. Watoto wangu wanatarajia kutoka kwa baba yao, lakini sitafanikisha chochote maishani kama mambo yataendelea hivi."

Grace Mugabe
Mke wa rais Mugabe, GracePicha: picture-alliance/ dpa

Manzou iko katika jimbo la Mashonaland ya Kati, ambalo gavana wake, Martin Dinha amesema anamuunga mkono Grace Mugabe kupata haki ya kulimiki shamba hilo kwa sasa. Gavana huyo amemtetea mke wa rais akisema, "Naichukia sana, kama mtu binafsi na kama waziri, tabia hii mbaya kabisa ya kumtangaza mke wa rais kama mtu mbaya. Kuna njama ya kisiasa kuharibu sifa ya kazi yake nzuri aliyoifanya. Neno Manzu katika lugha yetu ya kiafrika lina maana tembo, kwa hiyo watu wanaishi katika makazi ya wanyama. Napinga wazi kila wazo kwamba tunawafanyia watu ubaya."

Gavana mwingine mpya wa jimbo la Mashonaland Mashariki, Joe Biggie Matiza, amesema atachukua hatua kama hiyo kufikia mwisho wa mwezi huu. Hata hivyo mwanaharakati wa haki za binaadamu na mchambuzi wa masuala ya siasa Gabriel Shumba amesema kuzihusisha harakati za kuwafukuza wakulima wazungu na kundi la Mujuru ni njama ya kujipatia sifa kisiasa ya wale wanaotaka kuwafukuza wazungu. Shumba aidha amesema, "Wakulima wazungu wanajikuta wamebanwa katika kona kwa sababu wanamiliki raslimali inayohitajika sana."

Wakulima wazungu wanataka kukutana na waziri

Chama cha wakulima wanaofanya kilimo kwa ajili ya biashara, ambacho kwa kiwango kikubwa kinawawakilisha wakulima wazungu, kimetaka kukutana na waziri anayehusika na masuala ya ardhi wa Zimbabwe, Douglas Mombeshora, kuhusiana na kuwakufuza wakulima hao. Hayo ni kwa mujibu wa msemaji wa chama hicho, Hendricks Olivier. Olivier ameliambia shirika la habari la The Associated Press kwamba kuwafukuza wakulima weusi na wazungu haifai kwa sekta ya kilimo na panahitajika sera iliyo wazi.

Enteignung weißer Farmer in Simabwe
Wazungu wakifukuzwa shambani kwao "Peveril" (13.11.2001)Picha: AP

Waziri Mombeshora alisema hivi karibuni wakulima weusi wanaweza kuingia mkataba wa kufanya miradi ya pamoja na washirika wengine bila kujali rangi. Lakini makamu wa rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa baadaye alitoa ujumbe wa kutatanisha unaopingana na kauli ya waziri huyo, akionya juu ya kufukuzwa wakulima zaidi wazungu. Rais Mugabe mara kwa mara amezungumzia kupinga ushirika katika kilimo kati ya wakulima weusi wa wazungu.

Kwa mujibu wa chama cha wakulima wanaofanya kilimo cha biashara nchini Zimbawe kuna wakulima wazungu chini ya 300 kati ya idadi ya awali ya 4,500 waliokuwepo nchini humo. Mpango wa kuwafukuza wakulima uliowalenga wakulima wazungu kuanzia mwaka 2000 ulitetewa na rais Mugabe akisema ulihitajika ili kurekebisha hali ya kukosekana uwiano na usawa kuhusiana na masuala ya ardhi ulioanza tangu enzi ya utawala wa ukoloni, ingawa mpango huo ulilaumiwa kwa kuchangia kuvuruga usimamizi wa sekta ya kilimo ya Zimbabwe iliyokuwa tajiri.

Mwandishi: Josephat Charo/APE

Mhariri:Saumu Yusuf