1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakurdi na wanajeshi wa Iraq wasonga mbele Mosul

Yusra Buwayhid
24 Oktoba 2016

Wapiganaji wa kikosi cha Kikurdi - Peshmerga na vikosi vya Iraq, wamesonga mbele kuukaribia mji wa Mosul katika operesheni ya kuukomboa mji huo. Na, Waziri wa Ulinzi wa Marekani yupo ziarani nchini humo.

https://p.dw.com/p/2RbjP
Irak kurdische Kämpfer um Mossul
Picha: Reuters/A. Lashkari

Alfajiri ya leo, vikosi vya Kikurdi vimetangaza kupiga hatua na kuingia katika mji wa Bashiqa, uliopo kaskazini mashariki mwa mji wa Mosul. Vikosi hivyo vimesema vimefanikiwa kukamata vijiji kadhaa karibu na mji huo waliokuwa wakiulenga uliopo kaskazini mashariki mwa Mosul. Wapiganaji wapatao 10,000 wanapambana na kundi linalojiita Dola la Kiislam IS.

Vikosi vya Iraq navyo vimepambana jana na walenga shabaha pamoja na washambuliaji wa kujitoa muhanga wakijaribu kuusogelea mji wa Mosul, huku wakiwasaka wapiganaji wa  IS wanaofanya mashambulizi katika maeneo mengine nchini humo.

Jenerali wa jeshi la Iraq, Othman Al-Ghanimi hapa anelezea zaidi kuhusu operesheni hiyo:

"Tunaposema ni vita safi, tunamaanisha kwamba tunawalinda raia mbali na mapigano ya risasi. Tunajaribu kupunguza uwezekano wa majeruhi ya raia pia tunajaribu kulinda miundombinu isivurugwe," amesema Jenerali wa jeshi la Iraq, Othman Al-Ghanimi akielezea zaidi kuhusu operesheni hiyo.

Waziri Mkuu wa Uturuki, Binali Yildrim, amesema Wakurdi wa kundi la peshmerga waliomba msaada na Uturuki imeamua kuwapatia usaidizi wa kijeshi.

Iraq yakataa usaidizi wa Uturuki

Madai hayo ya Uturuki yanakuja siku moja baada ya serikali ya Iraq kukataa msaada wa Uturuki ambao ulipendekezwa kwao na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Ashton Carter aliyepo ziarani nchini Iraq katika eneo lenye Wakurdi wengi la Irbil, kutathmini hali inavyoendelea.

Irak Qayyarah Junge auf Fahrrad vor brennendem Ölfeld
Mtoto akiwa juu ya baiskeli nchini IraqPicha: Getty Images/C. Court

Operesheni hiyo ya mashambulizi iliyoanza Jumatatu iliyopita, ina lengo la kuukomboa mji wa Mosul kutoka mikononi mwa kundi la IS, hatua itakalolirudisha nyuma kundi hilo lilojitangaza kile inachokiita miliki ya khalifa nchini Iraq pamoja na nchi jirani ya Syria.

Carter amesema jana kuwa operesheni sambamba dhidi ya kundi la IS katika mji wa Mosul nchini Iraq na Raqqa nchini Syria ulikuwa ni mpango wao wa muda mrefu. Carter pia amekutana na kiongozi wa Wakurdi, Massud Barzani, na amempongeza kwa jitihada za Wakurdi katika mapambano hayo.

Maelfu ya wapiganaji, wakiwa ni pamoja na wanajeshi wa Iraq na Kikurdi wa kikosi cha peshmerga, wanashiriki katika operesheni hiyo kubwa ya kuukomboa mji wa Mosul.

Maafisa wa kijeshi wa Marekani wanakisia kwamba kuna wapiganaji wa IS kati ya 3,000 hadi 5,000 ndani ya mji wa Mosul na wengine kati ya 1,000 hadi 2,000 katika vitongoji vyake. Aidha raia milioni moja laki mbili wanakisiwa kuwepo ndani ya mji huo.

Wakati huo huo,mwakilishi wa UNICEF,  Peter Hawkins, amesema hali ni mbaya sana katika mji wa Mosul na timu za Umoja wa Mataifa zimetuma misaada ya msingi inayotarajiwa kuwatosha kwa wiki moja. Aidha amesema watoto wapo katika hatari ya kifo, ukatili wa kijinsia, kutekwa nyara pamoja na kuingizwa katika makundi ya wanamgambo.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/ape

Mhariri: Daniel Gakuba