1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

220209 G20 Berlin

Aboubakary Jumaa Liongo23 Februari 2009

Viongozi wa nchi sita zenye nguvu kiuchumi barani Ulaya, wamemaliza mkutano wao mjini Berlin, uliokua na madhumuni ya kuandaa msimamo wa pamoja wakati wa mkutano wa kundi la G20 London Uingereza

https://p.dw.com/p/GzT6
Kansela Angela MerkelPicha: AP

Viongozi hao  katika  mkutano huo uliomalizika jana walijadiliana jinsi ya kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi uliyoikumba dunia hivi sasa, kuhakikisha kuwa hali hiyo haijirudii tena, kwa kuweka taratibu mpya katika kusimamia masoko ya fedha.

Viongozi  wa  mataifa sita  hayo sita yenye uchumi mkubwa barani Ulaya walijadiliana na kukubaliana kufikiwa hatua mujarabu kukabiliana na hali hiyo.


Tangu kumalizika  kwa mkutano wa kwanza wa kilele wa mataifa yaliyoendelea kiviwanda na yale yanayoinukia  mwezi Novemba mwaka jana mjini Washington, Marekani, hali imezidi kuwa mbaya.


Akizungumza katika mkutano huo mwenyeji, Kansela Angela Merkel, alisema kuwa  mgogoro huo ambao haujawi kutokea kwa miongo kadhaa ni lazima usiruhusiwe kutokea tena.

„Tumekubaliana kwamba ni lazima tuimarishe taratibu za fedha na bila shaka  kuzisimamia  masoko yote ya fedha pamoja na wale wanaoshiriki, vilevile mifuko ya dhamana, mawakala pamoja na sekta nyingine binafsi´´


Katika mkutano wa kilele wa  kundi la nchi 20,  huko Washington, kulifikiwa makubaliano ya kuwepo mpango wa hatua za kuchukua, ambapo masuala muhimu 47 yalikubaliwa kushughulikiwa.

Makundi manne yaliundwa kuyashughulikia mambo hayo. Hata hivyo, hakuna jipya lililopatikana kwa upande wa Ulaya.

Kwa wakuu hao wa mataifa sita ya Ulaya,  jana walikubaliana kuchukuliwa hatua kali dhidi ya nchi ambazo zimekaidi kujiunga katika mfumo wa kubadilishana taarifa za  fedha pamoja na kuendeleza mfumo wa misamaha ya kodi.

Rais Nicolaus Sarkozy wa Ufaransa alisisitiza kuwekwa vikwazo dhidi ya nchi hizo zilizoendelea  kutokana na kukaidi kuachana na mfumo huo, na kusema kuwa mkutano utakaofanyika London wa G20 ni lazima uwe na mafanikio.


Rais huyo wa Ufaransa alisema kuwa washiriki wa mkutano huo wa London ambapo Rais Barack Obama atahudhuria watabeba jukumu la kihistoria na kuonya ya kwamba maamuzi mujarabu na thabiti ni lazima yafikiwe kwenye mkutano huo.

„Sote tunataka kwamba kunakuwa na mafanikio London. Na sote tunatambua ya kwamba hii ni nafasi yetu ya mwisho.

Sote tumekubaliana kwamba Ulaya inataka kuukarabati upya mfumo wote´´


Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, ambaye ndiye atakayekuwa mwenyeji wa mkutano huo wa April mbili, alisema kuwa kusaidia kuliimarisha shirika la fedha duniani, IMF, kutasaidia nchi za Ulaya ya Mashariki na Kati kukabiliana na mgogoro huo wa kiuchumi mnamo wakati ambapo benki za Ulaya Magharibi zinazoondoa mikopo yao.


„Tumeshuhudia kuchukuliwa hatua kubwa kabisa kuwahi kufanyika za kuupiga jeki uchumi.Tumeshuhudia kiwango kikubwa cha punguzo la kodi.Tumeshuhudia kuingizwa  kiwango kikubwa cha fedha katika mfumo wetu wa benki ili kuhakikisha mabenki yanaweza kufanya shughuli zake. Lakini leo hii tumeamua ya kwamba tunahitaji kufanya zaidi ya hayo kwa kushirikiana .Tunahitaji makubaliano mapya.Tunahitaji mapatano ya kibiashara kati ya nchi na mabara ya dunia hii ili siyo tu uchumi unyanyuke, lakini, kama alivyosema Angela Merkel,  ya kwamba mfumo wa uchumi katika siku zijazo utakuwa chini ya taratibu mujarabu kwa wote" 

Makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano huo wa Berlin yatajadiliwa na viongozi wa nchi zote 27 wananchama wa Umoja wa Ulaya mwezi ujayo, kabla ya kufanyika mkutano wa London wa kundi la G20.Ulaya katika kundi hilo inawakilishwa na Ujerumani, Uingereza, Ufaransa na Italia.