1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakuu wa nchi wa Ecowas kuijadili tena hali ya Guinea

Saleh Mwanamilongo
16 Septemba 2021

Marais wa Jumuiya ya ECOWAS wametarajiwa kukutana Alhamisi kujadili hatua za ziada kufuatia mapinduzi ya kijeshi nchini Guinea yaliyomwondoa rais Alpha Conde.

https://p.dw.com/p/40OMp
Guinea ECOWAS-Delegation in Conakry
Picha: Präsidentschaft Guineas

Mkutano huo wa wakuu wa nchi za Ecowas utatumika kutathmini ripoti ya ujumbe wa jumuiya hiyo ya kikanda uliotumwa nchini Guinea kukutana na watawala wapya wa kijeshi, kumtembelea Alpha Conde na kuhimiza kuundwa serikali ya mpito ya kiraia.

Mkuu wa ujumbe huo wa ECOWAS ambaye pia ni waziri wa mambo ya kigeni wa Ghana Shirley Botchwey amesema wakuu wa nchi watapitisha uamuzi juu ya hatua za kuchukua ili kuijeresha Guinea chini ya utawala wa katiba.

ECOWAS tayari ilichukua hatua wiki iliyopita kwa kusitisha kwa muda uachama wa Guinea kwenye jumuiya hiyo kama jibu kwa mapinduzi ya kijeshi iliyoyataja kuwa "ukiukaji mkubwa" wa mkataba wa kuanzishwa kwake.

''Waguinea wamechoka ''

Kufuatia shinikizo za kimataifa,jeshi linaanza Jumanne mikutano kuhusu mustakabali wa nchi hiyo. Chini ya uongozi wa Kanali Mamady Doumbouya, jeshi tayari  limekutana na maafisa kutoka vyama vya upinzani ,viongozi wa kidini, mabalozi wa nchi za kigeni na mashirika ya kiraia. Fode Mohamed Soumah, naibu spika wa zamani wa Bunge la Guinea amesema wamesubiri kuona hatua za mwanzo za viongozi wa kijeshi.

"Waguinea wamechoka. Waguinea wanataka matokeo ya haraka. Siwaombe viongozi wa kijeshi watatue shida zote, lakini angalau natumai wanaweza kuthamini na kutegemea ustadi kwa serikali kuanzia sasa.", alisema Soumah.

Serikali ya mpito ya kiraia ?

ECOWAS tayari ilichukua hatua wiki iliyopita kwa kusitisha kwa muda uachama wa Guinea
ECOWAS tayari ilichukua hatua wiki iliyopita kwa kusitisha kwa muda uachama wa GuineaPicha: Souleymane Camara/REUTERS

Mapinduzi ya kijeshi nchini Guinea yamepongezwa kwa tahadhari na wapinzani wengine wa muda mrefu wa rais aliyeondolewa Alpha Conde,akiwemo mpinzani maarufu Cello Dalein Diallo ambaye ameshindwa mara tatu na rais Conde katika chaguzi za rais nchini humo.

Wasiwasi unaongezeka kuhusu ni kwa namna gani jeshi hilo linaloongozwa na Mamady Doumbouya litaharakisha hatua ya kukabidhi madaraka kwa serikali ya mpito ya kiraia kama ilivyoagizwa na wasuluhisho wa jumuiya za kikanda na Kimataifa.

Doumbouya na wanajeshi wengine walio nyuma ya mapinduzi wamesema walimwondoa Conde kwa sababu ya wasiwasi juu ya umaskini na ufisadi, na kwa sababu alikuwa akihudumu muhula wa tatu madarakani baada ya kubadilisha katiba.

Hadi sasa hatma ya rais aliyepinduliwa Alpha Conde, haijafahamika. Ujumbe wa jumuiya ya Ecowas uliokuwa  mjini Conakry umesema wanajeshi bado wameweka masharti kadhaa kabla ya kumuachilia Conde mwenye umri wa miaka 83. Lakini hawakuyataja masharti yenyewe.