1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakuu wa nchi za Umoja wa Ulaya wakutana

Kabogo Grace Patricia25 Machi 2010

Viongozi hao wanakutana kwa siku mbili huko Brussels kutathmini njia za kupata suluhu ya mzozo wa kiuchumi wa Ugiriki.

https://p.dw.com/p/McPI
Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou (Shoto) na Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barroso.Picha: picture-alliance/dpa

Viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya wanakutana hii leo kujadiliana jinsi ya kupata suluhisho la tatizo la deni kubwa linaloikabili Ugiriki, ikiwa pia ni katika jitihada za kuzuia kushuka kwa thamani ya sarafu ya euro. Ujerumani kwa upande wake imeelezea msimamo wake kupinga kutolewa fungu la msaada wa kifedha kutoka kwenye umoja huo kwa ajili ya Ugiriki.

Mzozo wa deni la Ugiriki limelitikisa kundi la mataifa 16 yanayotumia sarafu ya euro na viongozi hao wako katika shinikizo kubwa la kuweka mfumo wa msaada ambao utayahakikishia masoko ya fedha kuhusu mpango wa kuiokoa Ugiriki. Nchi hiyo inahitaji kukopa kiasi euro bilioni 16 kati ya sasa hadi Mei 23 kwa ajili ya kukabiliana na deni hilo.

Lakini mgawanyiko bado upo miongoni mwa mataifa yanayotumia sarafu ya euro kuhusu jinsi ya kuisaidia Ugiriki, huku Ujerumani ikipinga mwito wa mataifa hayo kuisaidia Ugiriki moja kwa moja. Ujerumani inahofia kuwa hatua hiyo itakiuka masharti ya Umoja wa Ulaya na kuhimiza kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha hapo baadaye.

Akizungumza kabla ya mkutano huo, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ameliambia bunge la nchi hiyo-Bundestag kuwa hapingi juu ya Ugiriki kupatiwa msaada kama suluhisho la mwisho, lakini ameweka wazi kuwa makubaliano yoyote yale lazima yazingatie masharti ya Ujerumani na kulishirikisha Shirika la Kimataifa la Fedha-IMF.

Hata hivyo, baadhi ya wanachama wa kundi la mataifa yanayotumia sarafu ya euro na wanachama maarufu wa Benki Kuu ya Ulaya-ECB, wanahofia kuwa kitendo cha kuishirikisha IMF katika mzozo wa Ugiriki kitashusha thamani ya kundi hilo ambalo limeweza kusimama lenyewe kwa miaka 11.

Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou aliwaambia waandishi habari mjini Brussels, kuwa nchi yake itaendelea na mpango wake wenye kuumiza wa kupunguza matumizi ya bajeti yake, bila kujali kile kitakachojadiliwa katika mkutano huo wa siku mbili unaofanyika Brussels, Ubelgiji.

Kabla Bibi Merkel hajazungumza, Rais wa Benki Kuu ya Ulaya-ECB, Jean-Claude Trichet, alitangaza taarifa nzuri kwa Ugiriki, akisema kuwa benki hiyo itarefusha sheria za dhamana za mikopo hadi mwaka 2011, kimsingi sheria ambazo zilikuwa zimalizike muda wake mwishoni mwa mwaka huu.

Wakuu hao wa nchi za Umoja wa Ulaya wana wasiwasi kuwa matatizo ya deni la Ugiriki yanaweza yakasambaa katika nchi nyingine wanachama wa kundi la mataifa yanayotumia sarafu ya euro kama vile Ureno, Uhispania na Italia.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE)

Mhariri: Josephat Charo