1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walimwengu isipokua China wampongeza mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kwa mweaka 2010,Liu Xiaobo

Oumilkher Hamidou8 Oktoba 2010

Serikali kuu ya Ujerumani yaelezea matumaini yake kumuona Liu Xiaobo akiruhusiwa kwenda kuipokea mwenyewe tuzo yake ya amani

https://p.dw.com/p/PZah
Mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel Liu Xiaobo kabla hajafungwa December mwaka janaPicha: AP

Ulimwengu mzima umeusifu uamuzi wa kamati ya Nobel kumteuwa mwanaharakati wa haki za binaadam wa China,Liu Xiaobo kuwa mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel kwa mwaka huu wa 2010.Viongozi wa nchi kadhaa za Ulaya wametoa mwito mwanaharakti huyo aachiwe huru.

Viongozi ,tukiwatenga wale wa jamhuri ya umma ya China na Korea ya kaskazini na nchi nyenginezo zinazopinga mfumo wa kidemokrasi wameipongeza kamati ya Nobel kwa uamuzi wake.Muakilishi mkuu wa Umoja wa mataifa anaeshughulikia masuala ya haki za binaadamu bibi Navi Pillay amesifu "jaza kwa mwanaharakati mkuu wa haki za binaadamu."Liu Xiaobo ni mpiganiaji mkubwa wa haki za binaadam" amesema bibi Pillay wakati wa mkutano pamoja na waandishi habari hii leo.Tunapongeza mchango mkubwa wa wanaharakati wa haki za binaadam nchini China na katika nchi nyingi nyengine za dunia."Amesisitiza.

Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya José Manuel Barroso amempongeza mshindi huyo wa zawadi ya amani ya Nobel,anaetumikia kifungo cha miaka 11 jela nchini China,Liu Xiaobo akisema tuzo hiyo ni "risala ya nguvu kwa wanaharakati wote wa uhuru na haki za binaadamu ulimwenguni."

Spika wa bunge la ulaya Jerzy Buzek hakuchelea kuitaka serikali ya China imuachie huru haraka na bila ya masharti mwanaharakati huyo.

Serikali kuu ya Ujerumani pia inataraji mwanaharakati huyo ataachiwa huru ili aweze kuipokea mwenyewe tuzo yake ya amani.Msemaji wa serikali kuu ya Ujerumani Steffen Seibert anasema:

"Serikali ya shirikisho inampongeza kwa dhati mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel kutoka China.Ni jasiri anaetaka kusaidia kuipatia nchi yake demokrasia na mfumo unaoheshimu haki za binaadam,japo kama anajua ni utaratibu mgumu unaohitaji subira.Serikali ya Ujerumani inataraji ataachiwa huru ili aweze kuipokea mwenyewe tuzo hiyo.Serikali ya Ujerumani tangu zamani imekua ikipigania aachiwe huru na sasa pia itafanya hivyo hivyo."

Mwito wa kutaka aachiwe huru umetolewa pia na mke wa mshindi huyo wa zawadi ya amani ya Nobel, Liu Xia.Amesema anataraji jumuia ya kimataifa itaitumia fursa hii kuishinikiza China imuachie huru mumewe.

NO FLASH Wen Jiabao in Brüssel
Waziri mkuu wa China Wen Jiabao alipokuwa ziarani hivi karibuni mjini Brussels.Picha: AP

Jamhuri ya Umma wa China lakini ina mtazamo mwengine kabisa.Imeutaja uamuzi wa kamati ya Nobel kuwa ni mpujufu.Wizara ya mambo ya nchi za nje ya China imesema katika taarifa yake kutunukiwa zawadi hiyo mpinzani huyo wa serikali ni kinyume na malengo ya Nobel.China imesema pia uamuzi huo unaweza kuvuruga uhusiano kati ya China na Norway.

Wakati huo huo wakaazi wa Beijing wamesema vituo vya BBC na CNN vilisimamishiwa matangazo yao wakati kamati ya Nobel ilipokua ikitangaza uamuzi wake.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/Afp

Mpitiaji:Abdul-Rahman