1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walimwengu waanza kuitambua Kosovo

Hamidou, Oumilkher19 Februari 2008

Marekani,na nchi nyingi za ulaya zimesema zitafungua ofisi za ubalozi mjini Pristina

https://p.dw.com/p/D9fj
Bendera ya KosovoPicha: picture-alliance/ dpa




Marekani na nchi nyingi za Umoja wa ulaya zimeshaitambua Kosovo huru na nyengine zinajiandaa kufanya hivyo licha ya upinzani mkubwa wa Serbia ma onyo lililotolewa na nchi kadhaa zinazohisi tangazo la uhuru wa Kosovo litasababisha mashaka.


"Mkikifumbia macho kisa hiki,nani atakuhakikishieni kama na majimbo ya nchi zenu hayatajitangazia uhuru kwa njia kama hii ya kinyume na sheria?Amejiuliza rais Boris Tadjic wa Serbia mbele ya wanachama 15 wa baraza la usalama la umoja wa mataifa,katika wakati ambapo mjini Belgrade waziri mkuu Vojislav Kostunica ameamuru arejee nyumbani haraka balozi wa Serbia nchini Marekani.


Serikali ya Serbia imesema itawaamuru warejee nyumbani mabalozi wake wote walioko katika nchi zilizo na zitakazoitambua Kosovo.


Ufaransa ilikua ya kwanza kufanya hivyo ikifuatiwa na Uengereza,Italy,Australia,Indonesia na jumuia ya nchi za kiislam.Ujerumani huenda ikaamua kesho.


Waziri wa mambo ya nchi za nje Frank-Walter Steinemeier anasema:



"Nnataraji hali ya utulivu itarejee upya katika eneo hilo.Nnataraji jinamizi la zamani litatoweka na kuchomoza hali ya matumaini mema ya siku za mbele."


Akizungumza na waandishi wa habari mjini Daresalam nchini Tanzania,rais George w. Bush aliyekua ziarani nchini humo amesema tunanukuu"uhuru wa Kosovo utaleta amani katika eneo la Balkan.Sasa ni jukumu letu sote kuisaidia Kosovo iifikie amani-mwisho wa kumnukuu rais huyo wa Marekani aliyewakumbusha wakosovo wenye asili ya Albania watekeleze ahadi walizotoa za kuheshimu haki za wakaazi wote tangu wenye asili ya Kosovo mpaka wale ambao hawana asili ya eneo hilo.


Marekani sawa na nchi nyengine zilizoitambua Kosovo zinapanga pia kufungua ofisi zao za ubalozi mjini Pristina.


Katika wakati ambapo sehemu kubwa ya walimwengu wanawapongeza wakosovo kwa kujinyakulia uhuru wao,maandamano yamefanyika mjini Belgrade nchini Serbia kwenyewe na katika sehemu ya kaskazini ya mji uliogawika wa Mitrovica wanakoishi wakosovo wenye asili ya Serbia.Hakuna machafuko lakini yaliyoripotiwa.


Waserbia wameteremka majiani pia mjini Banja Luka,mji mkuu wa jamhuri iliyojitangaza wenyewe ya waserbia wa Bosnia-Srebska-huku waandamanaji wakizitupia mawe ofisi ndogo za ubalozi wa Ujerumani,Ufaransa na Marekani.

Waziri mkuu wa jamhuri ya Serbia Vojislav Kostunica amewatolea mwito waserbia waache kuandamana ili kuepukana na kitisho cha kuzuka machafuko na matumizi ya nguvu.Hata hivyo mkutano mkubwa wa hadhara utaitishwa mjini Belgrade alkhamisi ijayo.


Nchini Urusi magazeti hii leo yameutaja uhuru wa Kosovo kua "bomu lililoripuliwa na wanaopigania kujitenga jimbo hilo la Serbia."


Serbia na Urusi zimeshindwa jana katika juhudi zao za kutaka uhuru wa Kosovo ubatilishwe na baraza la usalama la umoja wa mataifa.

►◄