1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walimwengu wakumbuka zilzala ya Fukushima

11 Machi 2013

Leo hii Japan inakumbuka tetemeko la ardhi lillilopiga mashiriki ya nchi hiyo tarehe 11 Machi 2011 na kupelekea uharibifu mkubwa ambao haujashuhidiwa kwa kipindi cha robo karne nzima nchini humo.

https://p.dw.com/p/17usY
Mfalme Akihito na Malkia MichikoPicha: Reuters

Ni miaka miwili sasa tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi katika eneo la Fukushima ambalo Wajapan hawatalisahau katika maisha yao. Zaidi ya watu 19,000 walipoteza maisha, wengine kadhaa hawajuilikani walipo hadi sasa na maelfu wameendelea kuachwa bila makaazi hadi hivi leo.

Kumbukumbu zimefanyika katika miji mbalimbali mikubwa na midogo nchini humo. Maandamano makubwa yaliyowahusisha watu waliopoteza ndugu na jamaa zao katika tukio hilo la kihistoria yamefanyika katika mji mkuu Tokyo yakiongozwa na Mfalme Akihito na Malkia Michiko.

Maelfu ya wananchi wa Japan kutoka maeneo mbalimbali ya nchi hiyo wameinamisha vichwa vyao na kukaa kimya kwa dakika kadhaa kama ishara ya kukumbuka tukio hilo la mika miwili iliyopita.

Katika kumbukumbu hizo Mfalme Akihito amewataja watu walioathirika na tukio hilo na kusema kuwa hatasahau roho hizo wala watu wanaoishi katika mazingira magumu katika kambi za wakimbizi na sehemu nyingine.

Ujenzi mpya unazorota

Anti-Atom-Demonstrationen zwei Jahre nach Fukushima
Watu wanawakumbuka wahanga wa ajali ya FukushimaPicha: Reuters

Amesema kuwa kuwa kuna haja ya wananchi kupewa mazoezi ya kujiokoa wakati yanapotokea majanga ya kimaumbile kama hayo.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, ameahidi kujenga makaazi kadhaa ambayo yanahimili matetemeko ya ardhi na majanga ya kimaumbile kama hayo na kusema kuwa Japan imejifunza vya kutosha.

Kasi ya kuujenga mji huo bado ni ndogo sana, kwani zaidi ya watu 315,196 bado hawana makaazi ya kudumu na bado wanaishi katika kambi mbalimbali za kuhifadhia watu.

Bado jeshi la polisi nchini humo linaendelea kuwatafuta watu wanaodaiwa kupotea katika maeneo hayo ya pwani ambayo yaliathirika zaidi kwa Tsunami.

''Hatujapata ukweli wowote kwa muda wa mwaka mzima sasa," amesema afisa wa polisi nchini humo Toshiaki Okajima akiongea na shrika la habari la AFP, akiongeza kuwa bado kuna watu 1,300 hawajapatikana katika eneo la Miyagi pekee. "Lakini pia majonzi na mawazo ya familia zao bado hayajabadilika, na ndio maana jeshi la plisi linaendelea na zoezi la utafutaji miili hiyo iliyopotea," amesema afisa huyo wa polisi.

Mapema mnamo tarehe 11 Machi 2011, saa 8:46 mchana, Fukushima ilipigwa na tetemeko la ardhi lenye nguvu ya wastani wa 9.0 kwa kipimo cha Richter. Tangu siku hiyo, Fukushima haijawahi kurudi kwenye hali yake ya kawaida. Imebadilika milele!

Mwandishi: Hashim Gulana/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef