1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walinzi wa kampuni ya Blackwater wasamehewa

Josephat Charo30 Oktoba 2007

Walinzi wa kampuni ya kibinafsi ya ulinzi nchini Marekani Blackwater, wamepewa msamaha na hawatashtakiwa kutokana na kitendo cha kuwapiga risasi na kuwaua Wairaki 17 mjini Baghdad nchini Irak.

https://p.dw.com/p/C7g1

Walinzi hao wa kampuni ya Blackwater wamepewa msamaha na waongozaji mashtaka wakati wa uchunguzi uliofanywa na wizara ya mambo ya ndani ya Marekani katika kisa cha mauaji ya Wairaki 17 waliopigwa risasi mnamo tarehe 16 mwezi Septemba mwaka huu mjini Baghdad nchini Irak. Hayo yameripotiwa na gazeti la New York Times la Marekani hii leo.

Walinzi wa kampuni ya Blackwater USA walikuwa wakiulinda msafara wa magari yaliyokuwa yamewabeba maafisa wa wizara ya mambo ya ndani ya Marekani wakati walipowafyatulia risasi Wairaki hao katika barabara moja mjini Baghdad. Inasemekana walinzi hao walifyatua risasi bila kuchokozwa na hivyo kusababisha vifo vya Wairaki wasiopungua 17 katika hujuma hiyo.

Wachunguzi wa kitengo kinachohusika na ulinzi wa wanadiplomasia katika wizara ya mambo ya ndani ya Marekani waliwaahidi msamaha maafisa wa usalama wa kampuni ya Blackwater waliohusika katika kisa hicho cha mauaji ya Wairaki. Hatua hiyo ina maana kwamba maafisa hao hawatashtakiwa kwa jambo lolote la kweli walilolisema kwenye mahojiano yao na waongozaji mashitaka. Hayo yamesemwa na maafisa wa Marekani ambao hawakutaka majina yao yatajwe.

Vyanzo vya gazeti la New York Times vinasema haijabainika wazi ikiwa wachunguzi wa wizara ya mambo ya ndani wana mamlaka ya kutoa msamaha wa aina hiyo. Gazeti la Washington Post limeripoti kwamba kesi ya maafisa wa kampuni ya Blackwater imepelekwa kwa shirika la ujasusi la Marekani, FBI mapema mwezi huu, lakini maafisa wa shirika hilo hawawezi kutumia habari zilizokusanywa kutokana na mahojiano yaliyofanywa na wizara ya mambo ya ndani ambayo ina jukumu la kusimamia mikataba inayotolewa kwa makampuni ya ulinzi.

Mawakala wa shirika hilo wametaka kuwahoji tena maafisa wa usalama wa kampuni ya Blackwater ambao wengi wao inasemekana wamekataa. Afisa mmoja ameliambia gazeti la Washington Post kwamba maafisa wa kampuni ya Blackwater wamesisitiza waliahidiwa hawatashtakiwa kwa hiyo hawatakubali kuhojiwa. Hali hii itaifanya kazi ya shirika la ujasusi la FBI kukamilisha kesi hiyo kuwa ngumu.

Kiongozi wa kampuni ya Blackwater, Erik Prince, amekataa ripoti rasmi ya Irak inayosema mauaji ya Wairaki wote 17 yalifanywa bila kuwepo sababu. Badala yake bwana Prince anasisitiza kwamba maafisa wake walifyatuliwa risasi kabla kuwashambulia Wairaki hao.

Wizara ya mambo ya ndani ya Marekani inahitaji makapuni ya kibinafsi ya ulinzi kwa kuwa ina mawakala chini ya 1,500 ulimwenguni kote na jeshi la Marekani halina maafisa wa kutosha waliopokea mafunzo ya kuwalinda wanadiplomasia.