1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliouawa Yemen sasa wafikia 40

26 Mei 2011

Zaidi ya watu 40 wameuawa leo katika mapigano yanayotokea mitaani katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa, wakati maandamano ya kuupinga utawala wa miongo mitatu wa Rais Ali Abdullah Saleh yakigeuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.

https://p.dw.com/p/11Ois
Kiongozi wa kabila la Hashed, Sadiq bin Abdullah al-Ahmar (kulia)
Kiongozi wa kabila la Hashed, Sadiq bin Abdullah al-Ahmar (kulia)Picha: picture-alliance/dpa

Mamia ya waakazi wa Sanaa wamekuwa wakiukimbia mji huo kukwepa ghasia hizo, ambazo tangu kuanza kwake Jumatatu, zimeshagharimu maisha ya watu 80.

Mapigano kati ya majeshi ya serikali ya Rais Saleh na wapiganaji wa kabila lenye nguvu nchini humo la Hashed linaloongozwa na Sadiq al-Ahmar, yamesababisha umwagaji mkubwa wa damu kushuhudiwa tangu kuanza kwa maandamano dhidi ya serikali Januari mwaka huu. Sasa kuna hatari ya mapigano hayo kusambaa katika maeneo mengine ya nchi.

Wapiganaji waliovalia nguo za kiraia wameonekana wakitembeatembea katika baadhi ya wilaya za nchi hiyo, huku milio ya risasi ikisikika hapa na pale. Miripuko, moshi na hewa chafu vimetanda katika mji wa Sanaa, hasa katika eneo ambalo maelfu ya watu wanaotaka Rais Saleh kuondoka madarakani, baada ya utawala wake wa miaka 33 madarakani, bado wameweka kambi.

Miripuko katika mji mkuu wa Sanaa
Miripuko katika mji mkuu wa SanaaPicha: picture alliance / landov

Mapema Wizara ya Ulinzi ya Yemen ilisema kuwa watu 28 waliuawa kutokana na mripuko uliotokea kwenye ghala la silaha mjini Sanaa.

Ghala hilo la silaha lilikuwa likimilikiwa na kundi moja la kikabila linaloongozwa na familia ya Sadiq al-Ahmar. Waendesha mashtaka nchini humo wameagiza kukamatwa kwa kiongozi wa kundi hilo.

Kabila la Hashid analotokea al-Ahmar lina nguvu sana nchini Yemen na lina uwezo wa kukusanya na kufadhili maelfu ya wapiganaji. Imeelezwa kuwa kundi lake linalopigana na majeshi ya serikali ni shirikisho la wapiganaji.

Rais Ali Abdullah Saleh
Rais Ali Abdullah SalehPicha: dapd

Leo Rais Saleh leo aliagiza kukamatwa Sheikh Sadiq al-Ahmar pamoja na kaka zake tisa kwa tuhuma za uasi. Sheikh Sadiq, ambaye ni mmoja ya watoto 10 wa Sheikh Abdullah al-Ahmar, ambaye aliwahi kuwa mkuu wa bunge la Yemen na pia mshirika mkubwa wa Rais Saleh mpaka alipofariki mwaka 2007, ni mtu muhimu katika siasa za Yemen.

Sheikh Sadiq al-Ahmar alimrithi baba yake kuongoza kabila lao la Hashid na mwezi Machi mwaka huu akatangaza kuunga mkono waandamanaji wanaotaka Rais Saleh aondoke madarakani.

Mwandishi: Halima Nyanza/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef