1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wamarekani walia na matumizi ya nguvu ya polisi

5 Desemba 2014

Wimbi jipya na kubwa la maandamano katika mji wa New York na miji mengineyo siku 1 tu baada ya askari polisi mmoja wa kizungu kutajwa hana hatia ya kumuuwa bwana mmoja mweusi ambae hakuwa na silaha yeyote

https://p.dw.com/p/1Dzdi
Maandamano dhidi ya matumizi ya nguvu ya polisi huko BostonPicha: Reuters/B. Snyder

Kama katika kisa cha Michael Brown,kijana mweusi wa kimarekani aliyeuliwa Agosti tisaa iliyopita na askari polisi mweupe huko Ferguson,jopo la washauri mjini New York limehoji jumatano iliyopita "hakuna sababu ya kumwandama mahakamani polisi huyo wa kizungu aliehusika na kifo cha Eric Garner kilichotokea julai mwaka huu huko State Island.

Waziri wa sheria wa Marekani Eric Holder ameahidi hata hivyo uchunguzi wa kina na huru utafanyika kwa daraja ya taifa."Watu wataandamwa,ikilazimika" amesema Eric Holder anaehisi ni muhimu kurejesha imani ya wananchi kuelekea vikosi vya usalama.

Imedhibitishwa polisi wanatumia nguvu kupita kiasi

Waziri wa sheria alisema hayo Cleveland-katika jimbo la Ohio alipokuwa akizungumzia matokeo ya uchunguzi ulioanzishwa Machi mwaka 2013 na kuendelea mwezi uliopita kufuatia kisa cha polisi wa kizungu kumuuwa kijana wa miaka 12 mweusi aliyekuwa akichezea bastola bandia.Uchunguzi huo umedhihirisha "matumizi ya nguvu ya polisi yaliyokithiri."

USA Rücktritt von Justizminister Eric Holder
Waziri wa sheria Eric HolderPicha: Reuters/Gary Cameron

Kama ilivyokuwa siku moja kabla,maelfu ya watu waliandamana kuanzia saa za magharibi huko Manhattan na kuvuruga shughuli za usafiri.Wasi wasi ulikuwa mkubwa zaidi mnamo saa tano za usiku pale waandamanaji 3000 walipofika Times Square huku wakipaza sauti:"Mnawalinda akina nani"?Walikuwa wakiwaambia polisi waliokuwa wakijaribu kuwataka waondoke.Baadhi ya waandamanaji walikamatwa lakini hakuna machafuko yaliyoripotiwa.

Maandamano ya jana nchini Marekani yanasemekana kuwajumuisha watu wengi zaidi kuliko yaliyotangulia.Mjini Washington watu waliandamana mpaka katika wizara ya sheria,wakipitia ikulu ya Marekani kabla ya kukusanyika katika uwanja wa Washington Monument na kuvuruga pia shughuli za usafiri.

Huko Minneapolis dazeni kadhaa ya waandamanaji walizuwia shughuli za usafiri,baadhi yao wakilala chini barabarani huku wakizungukwa na polisi waliokuwa wakijaribu kuwaondowa.Maandamano yameripotiwa pia Chicago,Oakland na San Francisco.

Kutokana na ghadhabu za umma zilizosababishwa na uamuzi wa jumatano iliyopita,idara ya sheria mjini New York imeamua kuchapisha baadhi ya vifungu vya zoezi lililopelekea kutochukuliwa hatua za kisheria askari polisi wa kizungu.Kutokana na maombi ya mwendesha mashtaka wa eneo hilo,jaji Stephen Rooney wa State Island amesema jopo la washauri wamesikiliza ushahidi uliotolewa na watu 50 na kudurusu nyaraka 60 pamoja na madai mengineyo kabla ya kupitisha uamuzi wao.

Maisha ya mmarekani mweusi ni sawa na yale ya mwenzake wa kizungu

Kisa kilichonaswa katika filamu na mpita njia na kutangazwa katika mtandao kimetokea Julai 17,alipokamatwa Eric Garner baba mmoja wa familia ambae hakuwa na hata silaha lakini akituhumiwa kuuza sigara.

USA Begäbnis Eric Garner 3.12.
Mazishi ya Eric Garner huko New YorkPicha: Reuters/James Keivom/Pool/Files

Bwana huyo mnene na aliyekuwa akiugua maradhi ya pumu alitupwa chini na kugandamizwa na polisi kadhaa.Alikuwa akisikika akimwambia yule polisi aliyekuwa akimkaba roho,anashindwa kuvuta pumzi.Baada ya kupoteza fahamu akapelekwa hospitali na kifo chake kuthibitishwa.

Mashirika yanayopigania haki za kiraia yanatoa wito ateuliwe mwendesha mashtaka mkuu maalum kushughulikia matumizi ya nguvu ya polisi.

Mjini New York,meya Bill de Blasio aliyeingia madarakani mapema mwaka huu amesema askari polisi wote watapatiwa mafunzo mepya."Watu wanabidi waelewe maisha ya watu weusi na wa rangi ni muhimu sawa na yale ya wazungu" amesema.

Hata Hillary Clinton,anaetazamiwa kuwa mgombea wa kiti cha rais mwaka 2016 kwa tikiti ya chama cha Democratic ametoa wito mfumo wa sheria za jinai na mitindo ya polisi ifanyiwe mageuzi akisikitishwa na ile hali kwambva "weusi wanakamatwa na kusachiwa mara nyingi zaidi na polisi na kufungwa kwa muda mrefu zaidi kuliko wazungu."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu