1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wamarekani washangiria hukumu mauaji ya Floyd

Mohammed Khelef
21 Aprili 2021

Maelfu ya watu nchini Marekani wanaendelea kushangiria hukumu ya kwanza kumtia hatiani afisa polisi wa kizungu kwa mauaji ya mtu mweusi katika historia ya taifa hilo. 

https://p.dw.com/p/3sIyK
USA I Prozess um den Tod von George Floyd
Picha: Adrees Latif/REUTERS

 

Hata hivyo, Rais Joe Biden amesema kutiwa hatiani kwa Derek Chauvin kwa mauaji ya George Floyd kunaweza kuwa hatua kubwa katika vita dhidi ya ubaguzi wa kimfumo, lakini hakutoshi. 

Biden aliyekuwa akizungumza katika Ikulu ya White House akiwa na makamu wake, Kamala Harris, muda mchache baada ya mahakama kumtia hatiani Chauvin kwa mashitaka matatu ya mauaji, alisema Marekani haipaswi kutosheka na hukumu hiyo pekee, bali kusonga mbele hadi mfumo mzima uwe umebadilishwa. 

Viongozi hao wawili wamelitolea wito baraza la Congress kuyashughulikia haraka mageuzi ya polisi, ikiwemo kuidhinisha muswaada wa sheria uliopewa jina la Floyd aliyeuawa akiwa amegandamizwa goti shingoni mwezi Mei mwaka jana.