1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wamisri waitisha "Ijumaa ya Onyo la Mwisho"

15 Julai 2011

Ijumaa ya leo (15 Julai 2011), maelfu wa Wamisri wamefanya maandamano ya kitaifa wakidai mabadiliko ya haraka ya kisiasa na wakiulaumu utawala wa kijeshi kwa hatua za taratibu mno kuelekea mageuzi a kweli.

https://p.dw.com/p/11wBD
Bango linalosomeka "Mapinduzi Kwanza" katika mji mkuu, Cairo
Bango linalosomeka "Mapinduzi Kwanza" katika mji mkuu, CairoPicha: picture alliance/dpa

Maandamano ya leo yametayarishwa na makundi 28 ya wanaharakati. Wakiipa siku ya leo, jina la "Ijumaa ya Onyo la Mwisho", waandaaji wanasema lengo lao ni kulishinikiza Baraza Kuu la Kijeshi kuitikia matakwa yao.

Mjini Cairo, maelfu ya waandamanaji walikusanyika kwenye uwanja wa Tahrir, ambapo pamekuwa ni kituo cha kupigania demokrasia, tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Katika mji wa Suez, mamia ya waandamanaji walipiga makelele ya "Suez wameng'oa Mkuu wa Majeshi Hussein Tantawi" wakimaanisha kiongozi wa sasa wa Misri ambaye alikuwa waziri wa ulinzi wa Mubarak kwa miongo miwili mfululizo. Mamia mengine ya watu waliandamana katika mji wa pwani wa Alexandria.

Shirika la Habari la Serikali, MENA, limeripoti kuwa imamu aliyeongoza sala ya Ijumaa katika uwanja wa Tahrir, alitoa hotuba kali na kulitaka Baraza la Kijeshi liwachukulie hatua za kisheria mara moja, wale polisi waliofanya mauaji dhidi ya waandamaji katika siku 18 za mapinduzi hapo mwezi Februari.

Serikali imesema kwamba imepeleka magari ya kubebea wagonjwa na madktari kuwahudumia waandamanaji walio kwenye mgomo wa kula.

Mwandamanaji akibeba bango lililoandikwa "Dhidi ya Utawala wa Kijeshi" kwenye uwanja wa Tahrir
Mwandamanaji akibeba bango lililoandikwa "Dhidi ya Utawala wa Kijeshi" kwenye uwanja wa TahrirPicha: picture alliance/dpa

Miongoni mwa matakwa makubwa ya waandamanaji ni utawala kuacha kuwahukumu raia katika mahakama za kijeshi, kugawanywa kwa utajiri wa nchi na kuanzishwa kwa haraka kesi dhidi ya watawala wa zamani.

Waandamanaji wanalilaumu Baraza Kuu la Kijeshi kwa kung'ang'ania madaraka na kuchukuwa hatua za taratibu kuelekea mageuzi ya kweli. Baraza hili liliingia madarakani, baada ya waandamanaji kufanikiwa kumuondosha Rais Hosni Mubarak hapo mwezi Februari.

Dokta Saad Eddin Ibrahim, ambaye ni mwandishi na mwanaharakati nchini Misri, amekiambia kituo cha televisheni cha Al-Jazeera kwamba Baraza la Kijeshi haliwezi kubadilisha kitu, kwa kuwa lenyewe ni sehemu ya utawala uliopinduliwa.

"Wakati Hosni Mubarak alipolazimishwa kuondoka madarakani, alikasimu madaraka yake kwa Baraza Kuu la Kijeshi, ambalo aliliteua mwenyewe. Hili linaeleza kwa nini Baraza hilo linamchukulia Mubarak kwa huruma, kwa sababu utawala mkongwe bado haujatoweka moja kwa moja." Amesema Dokta Ibrahim.

Hapo jana, Waziri Mkuu Essam Sharaf aliamuru kufukuzwa kazi kwa maafisa wa ngazi ya juu wa polisi wanaoshukiwa kwa matumizi mabaya ya nguvu, huku Waziri wa Mambo ya Ndani, Mansour Essawy, akitangaza kuiunda upya idara ya polisi.

Mmoja wa waandamanaji katika uwanja wa Tahrir, Bola Abadou, amesema serikali haijawapa wanachokitaka.

"Matakwa yetu ni yale yale, lakini masharti ni tafauti, kwani tunazikataa hotuba zote, za waziri mkuu na baraza la kijeshi. Tunataka wayatekeleze matakwa yetu, kwa hivyo tutabakia hapa hapa uwanjani." Amesema Abadou.

Hata hivyo, vuguvugu la Ikhwanul-Muslimin halishiriki maandamano haya ya leo, likisema linaipa muda zaidi serikali kutekeleza matakwa ya waandamanaji.

Mkuu wa chama cha Uhuru na Haki, ambalo ni kama tawi la kisiasa la Ikhwanul-Muslimin, Mohammed Morsy, amesema kama matakwa hayo hayakutimizwa, ndipo watarudi tena uwanjani.

Hapo Jumatano, Baraza la Kijeshi lilitangaza rasmi kuyaunga mkono mapinduzi na malengo yake, lakini waandamanaji wanadai hatua zaidi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman