1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wamisri wapiga kura kuamua mustakabali wao

14 Januari 2014

Wamisri wameanza kuteremka vituoni kutoa maoni yao kuhusu katiba mpya, hatua inayoangaliwa kama kipimo cha umashuhuri wa jeshi lililomng'owa madarakani Mohammed Mursi, huku tayari kukiwa na taarifa za mashambulizi.

https://p.dw.com/p/1AqAy
Wamisri wanapiga foleni wakisubiri kupiga kuraPicha: Reuters

Jenerali Abdel Fatah al-Sisi, makamo waziri mkuu, waziri wa ulinzi na mtu pekee mwenye usemi katika nchi hiyo yenye wakaazi wengi zaidi miongoni mwa nchi za ulimwengu wa Kiarabu amewatolea wito wapiga kura milioni 53 "wateremke kwa wingi" vituoni na wapige kura ya "ndio".

Amesema pia atapigania kiti cha urais baadaye mwaka huu, ikiwa "umma utamtaka afanye hivyo" na kama jeshi litamuunga mkono.

Katiba mpya imetungwa na tume iliyoteuliwa na serikali ya mpito iliyoundwa na Jenerali al-Sisi tangu Julai tatu mwaka jana, baada ya kutangaza kupinduliwa na kukamatwa Mohamed Mursi, rais wa kwanza ambaye si mwanajeshi, aliyechaguliwa kwa njia za kidemokrasia nchini Misri.

Tangu wakati huo, na wakijivunia uungaji mkono wa wananchi walio wengi, utawala unaoongozwa na jeshi unamkandamiza kila unayemfikiria kuwa ni mfuasi wa Mohammed Mursi na hasa wale wa chama chake cha Udugu wa Kiislam.

Zaidi ya waandamanaji elfu moja wameuwawa miezi ya hivi karibuni na wafuasi wa Mursi kutiwa ndani kwa maelfu ingawa baadhi wanaendelea kuandamana kila kukicha huku Udugu wa Kiislam ukitoa wito wa kususiwa kura ya maoni ya katiba.

Ulinzi umeimarishwa

Sambamba na hayo mashambulizi yameongezeka ikiwa ni pamoja na mjini Cairo, huku wanamgambo wa itikadi kali wanaoshirikiana na al-Qaida waakidai kuhusika. Lakini serikali imekuwa ikiwatuhumu Udugu wa Kiislam kupanga mashambulizi kama hayo na imelitangaza kuwa ni miongoni mwa makundi ya kigaidi.

Ägypten Wahlen
Wanajeshi wanalinda usalama katika kituo cha kupiga kuraPicha: Mohamed El-Shahed/AFP/Getty Images

Leo asubuhi, muda mfupi kabla ya kura ya maoni kuanza, bomu limeripuliwa karibu na korti moja mjini Cairo, lakini hakuna aliyejeruhiwa. Baada ya mashambulizi hayo, watu kadhaa walikusanyika mbele ya korti hiyo wakionyesha mabango yenye picha za Jenerali al-Sisi.

Ili kulinda amani wakati wa zoezi hili la kura ya maoni litakalodumu siku mbili, serikali ya mpito imewaweka wanajeshi kati ya laki moja na 60 elfu na laki mbili kote nchini Misri.

Polisi na wanajeshi wamewekwa karibu na kituo cha kupiga kura katika shule moja mjini Cairo ambako akinamama kadhaa wamepanga foleni kusubiri kupiga kura.

Kura ya Maoni kama njia ya Kuhalalishwa

Baadhi ya mashirika ya haki za binaadamu yanaikosoa kura hii ya maoni inayofanyika katika hali ya woga na kukandamizwa upande wa upinzani, lakini idadi kubwa ya wananchi wanaonyesha kuunga mkono utawala mpya na Jenerali al-Sisi ambaye picha zake zimetundikwa katika kila pembe ya mji mkuu.

Ägypten Armeechef General Al Sisi 14.11.2013
Mkuu wa vikosi vya wanajeshi,jenerali Al SisiPicha: Reuters

Kwa maoni ya wataalamu, utawala mpya unaiangalia kura hii ya maoni kama njia ya kuhalalishwa kupitia vituo vya uchaguzi kile ambacho wapinzani wanakiita "mapinduzi ya kijeshi".

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef