1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanablogu wakutana mjini Nakuru Kenya kuzungumzia saratani

Amina Mjahid
31 Oktoba 2019

Wanablogu wa mji wa Nakuru wameshiriki kikao cha uhamasisho kupitia mitandao ili kutoa uhamasisho kuhusu ugonjwa wa saratani unaoendelea kuwaandama wengi nchini Kenya.

https://p.dw.com/p/3SHgv
Frankreich Krebsforschung im TIRO Labor
Picha: picture-alliance/BSIP/A. Noor

Ujumbe wa leo ulikuwa kuwahamasisha watu kuhusu ugonjwa wa saratani ili kuondoa dhana na unyanyapaa ulioko. Maurice Muturi, mwana blogu mbaye alihusika katika shughuli ya leo anaitaja mitandao kama jukwaa muhimu lenye ushawishi.

"Huu ukiwa mwezi wa kutoa ufahamu kuhusu saratani, tumepanga shughuli kadha wa kadha kwenye mitandao, mojawapo ikiwa kikao cha wana blogu ambacho kinafanyika leo, ambapo tunaenda kwenye mitandao na tunaanzisha mazungumzo ya kuwapa ufahamu watu kuhusu saratani. Hii ni muhimu kwasababu watu wengi siku hizi wako kwenye mitandao mara nyingi na wanapata taarifa nyingi kupitia njia hiyo. Huu ndio mpango bora zaidi wa kutoa uhamasisho kuhusu saratani tulioufikiria kwa sasa," alisema Muturi

Hii sio mara ya kwanza kwa wanablogu hawa kuandaa kikao kama hiki kwa malengo ya kutoa uhamasisho, ila leo walishawishika kuangazia saratani ambalo limekuwa janga linalowakosesha amani watu wengi nchini kwa sasa. Muturi anaeleza kuwa wamewashirikisha wauguzi kwenye shughuli hii kuhakikisha wanatoa ujumbe muafaka.

Saratani bado ni tishio duniani kote

Illustration zum Weltkrebstag am 4. Februar
Picha: picture-alliance/Pixsell/D. Puklavec

"Kwa kawaida hatuzungumzi kuhusu jambo ambalo hatulijui, kama ni jambo linalohitaji utaalam tunawahusisha madaktari na wauguzi walio na ujuzi kwa sababu ukienda mtandaoni na utoe taarifa za uongo utakuwa unamshawishi mtu kwa ujumbe usio sahihi."

Mary Gacheru ambaye ni muuguzi ameutaja huu kama wakati sawa kabisa kwa wadau kuungana kuondoa dhana potovu kuhusu saratani na kuwahamasisha umma kuhusu saratani.

Aidha, amezikosoa asasi zinazopinga shughuli inayoendelea ya kuwachanja watoto wa umri wa miaka 10 dhidi ya virusi vya papilloma (HPV), akisema chanjo hiyo ni salama na inalenga tu kuvilinda vizazi vijavyo dhidi ya saratani ya kizazi.

Kwa upande wake, Milcah Njeri, ambaye aligunduliwa kuwa na saratani ya kizazi mwaka 2008 na kupona baada ya matibabu, anawahimiza watu kuwa sio matukio yote ya saratani humalizikia katika mauti.

Katika Makala haya ya 11 tangu waanzishe vikao hivi, wanablogu hawa wanaazimia kutumia ushawishi kuielimisha jamii.

Wakio Mbogho, DW, Nakuru.