1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanachama wa Kadima nchini Israel wachagua kiongozi wao leo

Miraji Othman17 Septemba 2008

Chama cha Kadima nchini Israel kitakuwa na kiongozi mpya leo

https://p.dw.com/p/FJdj
Bibi Tzipi Livni, anayewania kuwa kiongozi wa Chama cha Kadima(kushoto), na waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert.Picha: AP


Wanachama wa chama tawala cha Kadima nchini Israel leo wanachagua kiongozi mpya wa chama chao. Wanaotiliwa dau kwamba watashinda ni baina ya waziri wa mambo ya kigeni, Bibi Tzipi Livni, na waziri wa usafiri,Schaul Mofaz. Pindi hamna kati ya watetezi atakayepata angalau asilimia 40 ya kura, basi itabidi ufanywe uchaguzi mwengine.

Pindi mtu ataamini uchunguzi wa maoni, basi matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa wazi hata kabla ya wanachama 74,000 wa Kadima kwenda kupiga kura leo kuamua nani awe kiongozi mpya wa chama chao. Yaonesha waziri wa mambo ya kigeni, Bibi Tzipi Livni, ana nafasi nzuri ya kushinda, hivyo kuchukuwa nafasi ya Ehud Olmert na huenda hata akaunda serekali mpya ya Israel.

Uchunguzi wa maoni unaonesha hadi asilimi 47 ya kura zitamuendea bibi huyo. Watetezi wengine wawili, waziri wa mambo ya ndani, Meir Shitrit, na waziri wa usalama wa umma, Avi Dichter, wako nyuma sana ya Bibi Livni. Mtetezi mmoja ndiye ambaye haujali uchunguzi wa kura hiyo ya maoni uliompa asilimia 30 ya kura. Yeye ni waziri wa usafiri, Shaul Mofaz, na ambaye, kwa kujiamini, alisema hivi:

" Naamini nitashinda katika duru ya kwanza ya uchaguzi kwa kujipatia asilimia 43.7. Kama nilivosema nitaunda serekali ijayo na kuupanuwa msingi wa serekali ya sasa."

Haijulikani wapi anakopata kujiamini huko, kwani hata washauri wake wa karibu wanaungama kwamba Shaul Mofaz, mwenye umri wa miaka 60, huichukulia siasa kama shughuli ya kijeshi. Shaul Mofaz, ambaye alizaliwa Iran na hapo kabla aliwahi kuwa mkuu wa jeshi na pia waziri wa ulinzi, ni wa upande wa wale wenye siasa za kichwa ngumu ndani ya Chama cha Kadima. Kwa mfano, linapokuja suala la mpango wa atomiki wa Iran, kama waziri pekee katika serekali ya Ehud Olmert, miezi iliopita alikikariri wazi wazi kutishia kuishambulia Iran. Shaul Mofaz ana imani kwamba msimamo huo mkali unaungwa mkono huko Israel na pia ndani ya Chama cha Kadima:

"wanachama wa Kadima wanataka dola ilio na nguvu na sio dola dhaifu, wanataka kiongozi aliye na nguvu na sio dhaifu. Wanachama wa Kadima, kama vile wale wa vyama vingine, leo wanatambuwa kwamba sisi hatuwezi kumudu kuwachaguwa watu wasiokuwa na uzoefu, wasiofahamu mambo na wasiokuwa na nguvu za kufikia maamuzi ili kuvishinda vitisho dhidi ya Israel."

Alikuwa anampigia kijembe Bibi Tzipi Livni. Waziri huyu wa mambo ya kigeni halifahamu suala la msingi la kuweko Israel. Mama huyu wa watoto wawili, ambaye katika ujana wake alikuwa kachero wa Idara ya Ujasusi ya Israel, hakubaliani na tuhuma hizo. Anasema, kama waziri wa mambo ya kigeni wa nchi yake mnamo miaka mitatu iliopita, ameshiriki katika maamuzi muhimu. Juu ya Vita vya Libanon, anasisitiza kwamba tangu vita hivyo vilipoanza, alishikilia vimalizwe mapema na akataka majeshi ya Israel yarejeshwe nyumbani.

Na Tangu pale ilipochapishwa ile ripoti juu ya Vita vya Libanon, yeye alitaka waziri mkuu Ehud Olmert ajiuzulu. Alitaka vivyo hivyo pale Ehud Olmert alipokuwa akihojiwa na polisi kwa shuku kwamba alipokea rushwa. Kwa Bibi Livni hatua yake hiyo ni kuisafisha siasa:

"Mtu lazima aseme ukweli kwamba tumevunjwa moyo. Watu wametuamini, walituchaguwa na hatujatimiza yale tulioahidi. Nafahamu na nasema leo, na mtu hawezi kusahihisha pale mtu hatokiri kile kilichotokea."

Bibi Livni anaahidi kutakuweko mwanzo mpya, bila ya kufichuwa fikra zake kuhusu mustakbali, hasa linapokuja suala la vipi amani itakavyokuwa na Wapalastina na kwa gharama gani yuko tayari kuilipia amani hiyo. Kuhusu Syria, bibi huyo yuko wazi zaidi. Ni wazi kwamba Israel lazima iirejeshe milima ya Golan, lakini Syria lazima ivunje mashikamano na wenye siasa kali, akikusudia kutoka Chama cha Hamas kupitia kile cha Hizbullah hadi Iran.

Pia Shaul Mofaz hasemi wazi juu ya mipango yake. Hapo zamani alipinga Israel kuondoka kutoka Ukanda wa Gaza na kuiwachia Milima ya Golan. Wakati Bibi Livni anataka kuweko uwazi zaidi na usafi katika siasa, Shaul Mofaz anahoji juu ya haja ya kuweko usalama, na anachukulia kwamba watu watamuamini yeye zaidi kuliko Bibi Livni, kwa vile aliwahi kuwa mkuu wa majeshi.

Pindi yule atakayeshindwa hataweza kuunda serekali imara ya mseto, basi itabidi uchaguzi mpya uitishwe na karata zichanganyishwe upya.