1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanadiplomasia wajadili hali ya usalama

Lilian Mtono22 Juni 2016

Wanadiplomasia waandamizi kutoka nchi sita, ikiwa ni pamoja na Marekani na Korea Kaskazini, wamekutana kwa mara ya kwanza baada ya miaka minne katika jukwaa linalojadili masuala ya usalama mjini Beijing, China

https://p.dw.com/p/1JBAY
Nordkorea Missile Tests
Picha: Ed Jones/AFP/Getty Images

Jukwaa hilo linafanyika wakati ambapo Korea Kaskazini ndio kwanza imefanya jaribio jengine la makombora ya masafa ya kati hivi leo.

Mazungumzo haya yasiyo ya kawaida yanayofanyika kwa siku mbili yanalenga kukabiliana na hali ya wasiwasi miongoni mwa mataifa, huku kukiwa na taarifa za majaribio ya makombora mawili ya masafa ya kati, yaliyofanywa na Korea Kaskazini hivi leo, na hii ikiwa ni kulingana na wizara ya usalama ya nchini Korea Kusini.

Makombora hayo yameripotiwa kwenda umbali wa kati ya kilomita 3,000 hadi 4,000 na yangekuwa na uwezo wa kulenga na kuipiga Marekani na kuweza kuifikia Alaska. Angalau kombora moja katika jaribio hilo lilishindwa, kwa mujibu wa ripoti ya maafisa wa Marekani na Korea Kusini ambao hawakutajwa majina yao. Makombora mengine manne yaliyofanyiwa majaribio awali pia yalifeli, ripoti hiyo ilisema.

Mazungumzo ya mwaka huu kuhusiana na mahusiano ya Kusini Mashariki mwa Asia ambayo, vyombo vya habari haviruhusiwi kuyatangaza, yamehusisha nchi zote ambazo zimehusika na jukwaa hilo linalijumisha nchi sita na yanalenga zaidi kuhusu mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini, China, Japan, Korea Kusini, Urusi na Marekani.

Msemaji kutoka wizara ya mambo ya nje ya Korea Kusini Cho-june Huke ameshutumu jaribio hilo la makombora na kusema linavunja makubaliano ya kiuasalama yaliyofikiwa na baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yanayozuia urushwaji wa makombora kwa njia za kiektroniki.

Aina ya makombora "Musudan" yaliyofanyiwa jaribio
Aina ya makombora "Musudan" yalilofanyiwa jaribioPicha: picture-alliance/dpa

Tayari mataifa yameanza kulaani hatua hiyo, Rais wa Korea Kusini, Park Geun-hyne amepinga hatua hiyo na kusema, kuendelea kwa majaribio hayo kutaifanya Korea Kaskazini kujiharibia yenyewe.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg ameshutumu vikali jaribio hilo, na kuitaka kuacha mara moja hatua hizo alizoziita kuwa ni za kiuchokozi. "Ninapinga vikali urushwaji wa makombora hayo mawili uliofanywa na Korea Kaskazini, amesema Stoltenberg kwenye taarifa yake.

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amelaani jaribio hilo
Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amelaani jaribio hiloPicha: picture-alliance/dpa/O. Hoslet

Japan kwa upande wake imesema, Hatua iliyofikiwa sasa na Korea Kaskazini ni ya kiwango cha juu katika mpango wake wa makombora, amesema Waziri wa usalama wa nchi hiyo, Generali Nakatani, na kuongeza kuwa inaongeza kitisho kwa nchi yake.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, John Kirby amesema, jaribio hili la sasa litasababisha kuongezeka kwa mikakati ya kidunia ya kukabiliana na mpango huo batili wa nyuklia wa Korea Kaskazini. "Tunalenga kuushinikiza zaidi Umoja wa Mataifa kuunga mkono juhudu za kimataifa za kurudisha nyuma juhudi za Korea Kaskazini juu ya mipango yake hiyo, amesema Kirk kwenye taarifa yake.

Chombo cha habari cha Korea Kusini Yonhap kimemkariri mmoja wa maafisa wa juu wa serikali nchini humo akisema jaribio hilo la pili linaashiria wazi kwamba nchi hiyo sasa ina uwezo mkubwa wa kiteknolojia.

Mwandishi: Lilian Mtono/DPA/AFP/RTRE.

Mhariri: Mohammed Khelef