1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanafamilia ya Kifalme kukosa Kombe la Dunia

14 Machi 2018

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May ametangaza kuwafukuza wanadiplomasia 23 wa nchi hiyo, kusistisha mawasiliano ya kiserikali na kufuta mwaliko kwa waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov.

https://p.dw.com/p/2uKKP
Großbritannien London - Premierministerin Theresa May
Picha: picture-alliance/empics/PA Wire

Hatua hiyo ni jibu la shambulio dhidi ya aliyekuwa jasusi wa Urusi nchini humo. Urusi imesema kuwa hatua za Uingereza dhidi yake ni za uhasama na zilizochukuliwa kwa pupa. 

May ameliambia bunge la Uingereza kuwa jaribio la mauaji dhidi ya Sergei Skripal na bintiye Yulia katika mji wa Salisbury unawakilisha matumizi ya Urusi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya Uingereza.

May alisema kuwa baada ya tukio hilo la kushangaza, uhusiano wa taifa lake na Urusi huwezi kusalia kama ulivyokuwa awali.

Ameongeza kusema, "kwa hivyo tutasitisha mawasiliano yoyote yaliyopangwa kati ya Uingereza na Urusi. Hii ni pamoja na kufutilia mbali ziara ya waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov hapa Uingereza. Nathibitisha kuwa familia ya kifalme na wanasiasa hawatahudhuria kombe la Dunia litakaloandaliwa Urusi." 

Wanafamilia ya Kifalme kukosa Kombe la Dunia, Urusi

Großbritannien London Queen Trooping the Colour
Baadhi ya wanafamilia ya Kifalme, UingerezaPicha: Reuters/T. Melville

May amesema mawaziri wa Uingereza na wanafamilia ya Kifalme hawatahudhuria mashindano ya kombe la soka la dunia yatakayofanyika nchini Urusi mwaka huu. Ametangaza hatua hizo baada ya Urusi kupuuza muda wa mwisho uliotolewa kueleza namna sumu iliyotengenezwa na Umoja wa Kisovieti ilivyotumika dhidi ya Sergei na Yulia Skripal.

Ubalozi wa Urusi jijini London umelaani misururu ya hatua hizo na kuzitaja kuwa zisizokubaliki, zisizo za haki na zenye maono mafupi. Taarifa hiyo imeongeza kusema kuwa wajibu wote wa kudorora kwa mahusiano ya Uingereza na Urusi uko mikononi mwa uongozi wa sasa wa Uingereza.

Ufaransa kusubiri ushahidi kabla ya kutoa maoni

Huku hayo yakiarifiwa msemaji wa serikali ya Ufaransa Benjamin Griveaux amesema, "ni mapema sana kwa Paris kutoa maoni kuhusu jaribio la jasusi huyo kuuawa kwa kuwekewa sumu katika taifa la Uingereza baada ya Uingereza kuishutumua Urusi."

Akitaja kitendo hicho kuwa kibaya Griveaux, amesema, "Ufaransa inasubiri ushahidi kabla ya kuchukua hatua zozote kwa mshirika wake Uingereza.

Griveaux amewaambia wanahabari muda mfupi baada ya waziri mkuu wa Uingereza Theresa kuwatimua wanadiplomasia 23 wa Urusi na kusitisha mazungumzo yoyote ya kibiashara na taifa hilo.

May amesema kuwa mustakabali wa kituo cha habari cha televisheni cha Uingereza sio wake bali ni wa shirika huru linalodhibiti vyombo vya habari nchini humo la Ofcom.

Ofcom lilionya Jumanne kuwa huenda likalinyanganya leseni shirika la Utanagazaji la Urusi la Russia Today(RT) iwapo serikali itabaini kuwa Urusi ilishiriki kwenye jaribio la mauaji ya jasusi huyo wa zamani.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Ap; Afp

Mhariri: Iddi Ssessanga