1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanahabari Uganda waachiliwa kwa dhamana

Lubega Emmanuel8 Februari 2019

Polisi Uganda imewaachia kwa dhamana wanahabari waliokamatwa kwa madai ya kukutikana na shehena ya dawa za serikali kinyume na sheria. Wanandishi watatu ikiwemo wawili wa shirika la habari la BBC pamoja na mke wa mmoja wao walikamatwa Jumatano usiku na walitarajiwa kufikishwa mahakamani alasiri Ijumaa kujibu mashtaka hayo.

https://p.dw.com/p/3D0kE


Kulingana na taarifa za polisi wandishi habari wawili wa kigeni wa shirika la BBC, mwenzao wa televisheni ya NBS Uganda, dereva wao pamoja na mke wa mmoja wao walikutikana na shehena ya dawa maalum za serikali usiku kwa kuamkia Alhamisi. 

"Operesheni ilifanywa na tukawakamata watu watatu wakinunua dawa maalumu. Tunamtafuta mshukiwa mwengine, atufahamishe jinsi dawa za serikali zilivyoishia nyumbani kwake," amesema Patrick Onyango, msemaji wa polisi.

Hata hivyo msemaji wa televisheni ya NBS Joe Kigozi amepinga kabisa madai yaliyotolewa dhidi ya waandishi hao. Amesema waandishi hao walikuwa wanashirikiana katika kufuatilia na kuandaa ripoti ya uchunguzi kuhusu jinsi dawa za serikali hutoweka kutokana na mienendo ya ufisadi iliyokithiri.

"Tunahitaji kufanya kazi yeu kama idhaa za habari, kufichua kashfa kama hizi na tulikuwa tunaelekea kukamilisha kazi yetu na ripoti yetu tutaitoa ikiwezekana ,"amesema Kigozi.

Habari kwamba waandishi hao walikuwa wamepangiwa kufikishwa mahakamani Ijumaa, kujibu mashtaka ziliwasababisha wanahabari wengi asubuhi Ijumaa kufikia uamuzi wa kuandamana hadi mahakamani wakiwa wamevalia mavazi meusi kuonyesha mshikamano na wenzao waliokamatwa wakifanya kazi yao kwa njia wanaoataja kuwa halali bila kuvunja sheria yoyote. Hata hivyo mipango hii imevunjiliwa mbali baada ya polisi kuwaachia washukiwa wote kwa dhamana.

"Hawana sababu ya kukiuka haki za wanahabari kwa kuwavizia nyumbani kwao, wangewakamata kazini kwao ," alieleza Robert Sempala, mratibu wa mtandao wa haki za wanahabari Uganda.

Wakili wa wanahabari hao Medard Segona amesema kuwa huenda polisi wamejikuta mashakani baada ya ukweli kufichuliwa, na kwamba hata wale waliosababisha wanahabari hao kukamatwa ni washukiwa katika kashfa ya wizi wa dawa za serikali. Wizi huu mara nyingi unadaiwa kuwa chanzo cha uhaba wa dawa katika vituo vya afya vya serikali ikisemekana  huunzwa nchi jirani baada ya kuporwa. Washukiwa wataripoti kwenye kituo cha polisi tarehe 18 mwezi huu.

Mwandishi: Emmanuel Lubega

Mhariri: Yusuf Saumu