1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Congo na Uganda wapambana Ziwa Edward

Josephat Charo
6 Julai 2018

Mapigano kati ya majeshi ya wanamaji wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na wale wa Ugada kwenye Ziwa Edward wilayani Beni katika Mkoa wa Kivu Kaskazini yanaripotiwa kuuwa watu wapatao sita.

https://p.dw.com/p/30vu2
Kongo 2012 - Soldaten der M23-Rebellenbewegung
Picha: Imago/Kyodo News

Akizungumza na kituo cha redio cha RTR kwa njia ya simu, mwenyekiti wa mashirika ya kiraia katika mji mdogo wa Kyavinyonge, Samy Muloko, alisema kuwa tangu majuzi wanamaji wa jeshi la Uganda waliteka mitumbwi ya wavuvi kumi na wanane wa Kongo, na mingine saba hapo jana.

Hali hiyo, kwa mujibu wa Muloko, ilipelekea wanamaji wa jeshi la Congo walioko katika mji mdogo wa Kyavinyonge kupiga doria katika Ziwa Edward na ghafla wakakutana na wanajeshi wa Uganda, na ndipo makabiliano yakaanza kati yao:

Makabiliano ya jana kwenye Ziwa Edward yaliyopelekea kuuawa kwa wanajeshi watano na raia watatu upande wa Uganda, kwa mujibu wa duru za mashirika ya kiraia, ni ya kwanza ya aina yake kutokea katika ziwa hilo kwa miaka kadhaa sasa.

Kikawaida, wanaposhikwa wavuvi wa pande zote mbili, yaani DRC na Uganda, kuna tume zinazohusika na kufuatilia mikasa ya aina hiyo, ambazo baadaye hufanikisha kuachiwa kwao huru. Lakini hadi sasa hakuna upande wowote uliozungumzia lolote kuhusu mkasa huo wa jana.

Mapambano na waasi wa ADF

Huku hayo yakiendelea, jeshi ya Congo lilipambana jana na waasi wa ADF kutokea Uganda katika Bonde la Mualika wilayani Beni.

Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi, katika operesheni hiyo dhidi ya ADF, waasi tano waliuawa na silaha moja aina ya AK47 kuchukuliwa na majeshi ya Congo.

Kapteni Mack Hazukay alisisitiza, kuwa walipokuwa wanapambana na waasi wa ADF, pia kulikuwa na wapiganaji wa Maimai kutoka kundi la UPLC ambao waliwashambulia wanajeshi katika kijiji cha Kanyihunga, wilaya ya Beni.

Kwa mujibu wa KapTeni Hazukay, wapiganaji watatu wa Maimai waliuawa, na kwamba operesheni za safishasafisha zinaendelea:

Kwa mujibu wa wachambuzi wa mzozo huu wa mashariki ya Kongo, harakati za wapiganaji wa kijadi wa Maimai katika wilaya ya Beni, zinaonekana kupunguza nguvu ya majeshi ya Congo katika vita vyake dhidi ya waasi wa ADF, na madhara ni kuuawa kwa raia wa kawaida na ADF katika maeneo mbalimbali. Swali ni je, Maimai wanawaunga mkono waasi wa ADF kutoka Uganda au la?

Mwandishi: John Kanyunyu/DW Beni

Mhariri: Mohammed Khelef