1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Congo matatani

Mjahida19 Novemba 2015

Ofisi ya haki za binaadamu ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imetoa ripoti inayosema wanajeshi wa nchi hiyo wamewabaka wanawake 14 ndani ya siku tatu Mashariki mwa Congo.

https://p.dw.com/p/1H92P
Wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya CongoPicha: Alain Wandimoyi/AFP/Getty Images

Ukatili huo unasemekana kufanyika katika eneo la Kalehe, mkoa wa kivu ya kusini kati ya tarehe 20 hadi 22 mwezi Septemba, wakati wanajeshi wa Congo walipokuwa wanaendesha msako wa kumtafuta kiongozi wa waasi.

Maovu hayo ni miongoni mwa msururu wa unyanyasaji wa kingono uliofanyika Mashariki mwa Congo eneo ambalo maelfu ya waasi wanapoendesha shughuli zao na mamilioni wameuwawa kutokana na njaa na magonjwa wakati wa vita vya kati ya mwaka 1998 na 2003.

Hata hivyo makundi ya kutetea haki za binaadamu pamoja na mashirika ya kiraia nchini humo yamekuwa yakiishutumu serikali na waasi kutumia ubakaji kama silaha katika vita. makundi hayo yanataka serikali kuchukua hatua dhidi ya wanajeshi wanaohusika na matendo hayo maovu.

Aidha Mkurugenzi wa ofisi ya Umouja wa Mataifa inayoshughulikia aki za binaadamu Jose Maria Aranaz, amesema tukio hili ni baya zaidi kuwahi kusajiliwa mwaka huu iliowajumuisha wanajeshi wa Congo.

Baadhi ya wanajeshi wa Congo
Baadhi ya wanajeshi wa CongoPicha: Reuters/Kenny Katombe

Jose Maria hata hivyo amesema amefurahishwa na jibu la serikali baada ya ofisi yake wiki hii kuifahamisha serikali hiyo kile kinachotokea, na kwamba ana imani serikali itashikilia sera yake ya kutokomeza visa vya unyanyasaji wa kingono.

Lambert Mende asema ripoti iliyotolewa inalenga kuichafua Congo.

Korti ya kijeshi Mashariki mwa mkoa wa Maniema mwezi uliyopita ilimshitaki afisa wa polisi aliyekuwa na cheo cha juu kwa makosa ya uhalifu dhidi ya binaadamu ikiwemo ubakaji uliotekelezwa na kitengo chake mwaka 2012. Wakati huo huo serikali ya Congo imeongeza idadi ya kesi za unyanyasaji wa kingono lakini wahusika kufunguliwa mashitaka ndio imekuwa changamoto kuu.

Kwa upande mwengine Msemaji wa serikali ya Congo Lambert Mende amesema hajui lolote juu ya makosa yaliyoorodheshwa katika ripoti hiyo lakini moja kwa moja akaushutumu ofisi ya Umoja wa Mataifa kwa kuipaka tope Congo kwa kuitoa hadharani ripoti hiyo badala ya kuiwasilisha mahakamani.

Aidha wanadiplomasia wa ufaransa wamesema jeshi la Congo halipaswi kuwa miongoni mwa ujumbe wa MINUSCA kwa sababui ya shutuma zinazowakabili. kwa sasa takriban wanajeshi 400 wa Congo wapo katika ujumbe huo wa Minusca unaojumuisha wanajeshi 9000.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman