1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Israel na wale wa Libnan wafyetuliana risasi

Oummilkheir8 Februari 2007

Wanajeshi wa Umoja wa mataifa wamepelekwa katika eneo la mpakani la Israel na Libnan

https://p.dw.com/p/CHKX
Vikosi vya kulinda amani vya UNIFIL nchini Libnan
Vikosi vya kulinda amani vya UNIFIL nchini LibnanPicha: AP Graphics

Vikosi vya kulinda amani vya umoja wa mataifa vimewekwa katika mpaka wa Libnan na Israel hii leo,baada ya wanajeshi wa Libnan na wale wa Israel kufyetuliana risasi jana usiku.Hii ni mara ya kwanza kuripuka balaa kama hilo tangu vita vilivyoanzishwa na Israel dhidi ya Hisbollah, kumalizika msimu wa kiangazi uliopita.

Kisa hicho kimejiri katika eneo la mpakani la Maroun-ar-Raas, lililozungushwa senyenge kusini mashariki ya Libnan.

Wanajeshi 200 wa Umoja wa mataifa ambao ni sehemu ya wanajeshi 12 elfu waliopewa jukumu la kusimamia amani kusini mwa Libnan wameshapelekwa katika eneo hilo na kuwekwa chini ya uongozi wa kijeshi wa Ufaransa.

“Jeshi la Israel na vikosi vya Israel wamefyetuliana risasi katika eneo la mstari wa buluu.Tukio hilo limesababishwa na jeshi la Libnan baada ya tinga tinga la Israel kuuvuka mstari huo uliozungushwa senyenge-kwa kile kinachodhihirika kua jaribio la kuchumbia miripuko” ameeleza msemaji wa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa,Milos Strugar.

Tukio hilo linalotajwa na UNIFIL kua ni “la kuchukiza” limemalizika saa sita za usiku bila ya kuwepo majeruhi.

Mjini Jerusalem,mkuu wa vikosi vya wanaanga vya Israel,jenerali Alon Friedman,amesema Israel itazidisha harakati zake katika anga ya Libnan.”Tunataraji hali itatulia lakini tunajiandaa kwa kila kitakachotokea” amesema jenerali Friedman.

“Amri za kufyetua risasi zimebadilika tangu vita vilipomalizika.Tunaweza kumpiga risasi yeyote atakaetufyetulia risasi,yeyote anaebeba miripukio au yeyote ambae tunahisi ni kitisho kwa usalama wetu.” Amesema hayo jenerali Friedman.

Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert na waziri wa ulinzi Amir Peretz,ambao wote wawili wanatiwa kishindo wajiuzulu kutokana na jinsi vita vya Libnan vilivyopita,wanatazamiwa kukutana na maafisa wa ngazi bya juu wa kijeshi hii leo na mawaziri kuzungumzia suala hilo.

Kwa mujibu wa vikosi vya usalama vya Libnan,wanajeshi wao wamefyetua risasi baada ya kifaru cha jeshi la Libnan kuhujumiwa kwa kombora la Israel.

Eneo hilo la mstari wa buluu lililozungunshwa senyenge limetengwa na Umoja wa mataifa tangu mwaka 2000.

Israel imekua kila wakati ikiwatzuhumu wanamgambo wa Hisbollah kutega miripuko katika eneo hilo.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Philippe Douste-Blazy ameutaka uongozi wa vikosi vya umoja wa mataifa vya kusimamia amani Libnan vichunguze haraka kadhia hiyo.