1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapambano makali yatarajiwa Msumbiji

Josephat Charo
25 Agosti 2020

Ufanisi wa waasi wenye misimamo mikali ya kiislamu kuiteka na kuidhibiti bandari ya kaskazini mwa Msumbiji kunaiashiria serikali, mataifa jirani na ulimwengu mzima kuwa Afrika ina eneo lengine linalokabiliwa na uasi.

https://p.dw.com/p/3hUGp
Mosambik Mocimboa da Praia | Soldaten in Mosambik | Islamisten
Picha: Getty Images/AFP/A. Barbier

Makabiliano makali yanatarajiwa huku serikali ya Msumbiji ikiviandaa vikosi vyake kuiteka tena bandari ya Mocimba da Praia, bandari ya kimkakati kaskazini mashariki mwa taifa hilo ambayo ilitekwa na wanamgambo wa kiislamu mapema mwezi huu.

Kundi la wanamgambo wa kiislamu walionesha viwango vipya vya mipango, mikakati, nguvukazi na silaha katika mapambano ya siku kadhaa kati yao na vikosi vya serikali ambapo hatimaye walifanikiwa kuidhibiti bandari hiyo mapema mwezi huu.

Ushindi wa wanamgambo hao huko Mocimboa unaongeza orodha ya vikwazo vinavyoukabili uwekezaji wa mabilioni ya dola kutumia hazima kubwa ya gesi asilia kaskazini mwa Msumbiji.

Mocimboa, inayopatikana kaika mkoa wa Cabo Delgado, kaskazini mwa Msumbiji, ni bandari ya karne iliyopo katika njia za biashara katika bahari ya Hindi na karibu na mpaka wa Tanzania. Hii ni mara ya tatu mji wa Mocimboa wenye wakaazi takriban 30,000 kudhibitiwa na waasi na ni kwa kipindi kirefu kabisa kufanikiwa kufanya hivyo.

Mtaalamu wa historia katika chuo kikuu cha Belfast, Eric Morier-Genoud, amesema kuanguka kwa Mocimboa da Praia ni ushindi mkubwa wa kimkakati kwa waasi. Mtaalamu huyo aidha amesema ushindi huo pia wa kibinafsi kwa waasi hao kwa kuwa wengi wanatokea mji huo na walirejea kwa hali tofauti kila mmoja akitaka kupata ushindi na kuonesha ari na ujuzi wa hali wa juu kivita.

Waasi wamedhihirsha uwezo wao mkubwa

Waasi walipambana na majeshi ya serikali mjini Mocimboa kuanzia Agosti 5 hadi Agosti 10. Waliuvamia msafara wa magari ya wanajeshi waliokuwa wakielekea mjini humo kutokea kambi ya jeshi ya Mueda. Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa makuruta 50 wenye umri mdogo waliuliwa katika uvamizi huo katika kijiji cha Awasse.

Wanajeshi wa serikali walisaidiwa na helikopta zenye silaha kutoka kwa kampuni ya Dyck Advisory ya Afrika Kusini, lakini jitihada zao zilikwamishwa na haja ya kurejea mji mkuu wa mkoa, Pemba, kujaza mafuta. Kwa mujibu wa shirika la habari la Zitamar, helikopta hizo pia zilidondosha mahitaji na silaha mbali na maeneo zilikohitajika.

Waasi wameushikilia mji huo kwa wiki mbili na panatarajiwa kutokea mapambano makali kati yao na wanajeshi. Morier Genoud anasema jeshi litaukomboa mji wa Mocimboa da Praia lakini swali ni lini na kivipi. Na hata wakiukomboa, swali lengine linaloulizwa ni je watafanikiwa kuudhibiti kwa muda gani. Huku laini zote za simu na huduma za mawasiliano ya intaneti kwenda Mocimboa zikiwa zimekatwa, ni vigumu kubashiri watakachokifanya waasi hao.

Mbali na kuendelea kupokea msaada kutoka kwa kampuni ya Dyck ya Afrika Kusini, Msumbiji imejiepusha kuomba msaada kutoka nje na inaonekana itaendelea na msimamo wake huo hata inapochukua urais wa kupokezana wa jumuiya ya kiuchumi ya kanda ya kusini mwa Afrika, SADC.

Waziri wa ulinzi wa Msumbiji, Jaime Neto, amesema hivi karibuni kwamba msaada pekee nchi hiyo inayoomba kutoka kwa majirani zake ni usimamizi na upekuzi mipakani kuwazuia wahalifu kuingia katika taifa hilo.

(ap)