1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa UN waondoka mpakani mwa Eretrea na Ethiopia

Saumu Mwasimba31 Julai 2008

Baraza la usalama la Umoja wa mataifa limepiga kura ya kuondoa wanajeshi wake wote wa kuweka amani katika eneo la mzozo la mpaka kati ya Eritrea na Ethiopia

https://p.dw.com/p/Eo43
Kikosi cha kuweka amani cha UNMEE katika mpaka wa Eretrea na EthiopiaPicha: UN/DPI PHOTO

Hata hivyo baraza hilo limezitolea mwito pande zote mbili kujizuia kutumia nguvu.Muda wa Kikosi cha wanajeshi 1700 wa umoja huo unamalizika hii leo.

Baraza hilo la usalama la umoja wa mataifa lenye wanachama 15 lilipitisha hapo jana jioni azimio la kusimamisha shughuli za kuweka amani za kikosi hicho chenye wanajeshi 1700 cha UNMEE kilichoko katika eneo la mpaka kati ya Eretrea na Ethiopia.Azimio hilo nambari 1827 linatoa mwito kwa pande hizo mbili kujizuia kutumia nguvu au kutoleana vitisho au hata uchokozi wa kijeshi.

Hatua ya baraza la usalama la umoja wa mataifa imekuja kufuatia uamuzi wa Eretrea wa kuweka vizuizi dhidi ya wanajeshi hao na Ethiopia kukataa kuutambua uamuzi uliotolea na jopo la kimataifa la kuweka mipaka ambao uliamua mji wa mpakani wa Badme kuwa ni milki ya Eretrea.Akitangaza uamuzi huo wa baraza la usalama umetangazwa na msemaji wa katibu mkuu Yves Saracovice.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon hata hivyo ameelezea matumaini yake kwamba pande zote mbili zitafainikiwa kuondoa tofauti zao na kujenga mazingira yanayofaa kuleta uhusiano wa kawaida baina yao ambao ni muhimu kwa amani na usalama katika eneo hilo.

Itakumbukwa kwamba chini ya makubaliano ya mwaka 2000 ya mjini Algieirs ambayo yalimaliza vita vya miaka miwli vya mpakani,nchi hizo mbili Eretrea na Ethiopia ziliahidi kwamba zitakubaliana na uamuzi utakaopitishwa na jopo hilo la kimataifa kuhusu maeneo hayo ya mzozo.

Lakini kwa upande mwingine akionya juu ya kitisho kilichoko kati ya nchi hizo mbili Nick Bernback mkuu wa masuala ya umma katika idara ya vikosi vya kuweka amani vya Umoja wa mataifa amesema'' hali ya mvutano kati ya nchi hizo mbili bado ipo na kila nchi imeweka wanajeshi wake katika maeneo ya mpakani kwenye mji wa Badme''

Balozi wa ubelgiji katika umoja wa mataifa Jan Grauls amesema jeshi hilo la Umoja wa mataifa linaondolewa kwa bahati mbaya sio kwa sababu muda wake umetimizwa lakini kwasababu muda wake umekuwa vigumu kutimizwa.

Ameongeza kusema kuwa serikali za mjini Asmara na Addis Ababa zinaweza kuamua kuimaliza hali hii kwa kukomesha mivutano yao na badala yake wafikirie na kuamua kwa maslahi ya wananchi wao.

Aidha amesema nchi hizo ikiwa zinataka amani katika eneo zima la upembe wa Afrika zinabidi kufuata njia ya mazungumzo.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon akizungumzia kuhusu hali hiyo ameelezea matumaini yake kwamba pande zote mbili zitafanikiwa kuondoa tofauti zao na kujenga mazingira yanayofaaa kuleta uhusiano wa kawaida baina yao ambao ni muhimu kwa amani na usalama katika eneo hilo.

Kwa upande wake naibu balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa mataifa Jean Pierre Lacroix amewaambia waandishi wa habari kwamba Eritrea ndio chanzo cha kikosi cha UNMEE kutoweza kuendelea kuweka amani.