1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi waahidi mageuzi ya demokrasia Misri

14 Februari 2011

Viongozi wapya wa kijeshi nchini Misri wanajaribu kurejesha hali ya kawaida nchini humo, baada ya rais Hosni Mubarak kujiuzulu Ijumaa iliyopita.Bado haijulikani iwapo viongozi hao wapya watakujapata imani ya umma.

https://p.dw.com/p/R0gr
Stichwort: Tahrir-Samstag Titel: Am Tahrir-Platz wird sauber gemacht und demonstriert. Beschreibung: Menschen auf den Tahrir-Platz räumen auf. Andere demonstrieren. Auf dem Transparent steht: "Eilmeldung: das Volk hat das Regime gestürzt." Aufnahmedatum: 12.02.2010 Aufnahmeort: Kairo Rechte: Khalid El Kaoutit Die Deutsche Welle darf dieses Bild verwenden.
Uwanja wa Tahri - Kitovu cha maandamano ya upinzani CairoPicha: Khalid El Kaoutit

Kwa mara ya kwanza, baada ya majuma mawili,hali ya kawaida ilianza kurejea pole pole katika uwanja wa Tahrir ulio katikati ya mji mkuu Cairo. Mapema hiyo jana, eneo hilo lilifunguliwa kwa usafiri wa kawaida baada ya maelfu ya watu kumiminika kwenye uwanja huo usiku wa kuamkia Jumapili kusherehekea kuondoka kwa Mubarak. Mapema jana asubuhi, wanajeshi walianza kuondosha mahema ya waandamanaji na kulizuka mapambano ya hapa na pale baada ya baadhi ya waandamanaji kukataa kuondoka. Wengi wao lakini waliondoka wakisema kuwa wameridhika.

"Tumefikia lengo letu, tumeiangusha serikali. Yeyote yule atakaeshika madaraka, atapaswa kutimiza madai yetu: kuwepo haki na uhuru.

Lakini wanaharakati wengine waliamua kubakia huko huko, baada ya viongozi wa kijeshi kutangaza kuwa mawaziri wa serikali ya zamani watabakia madarakani mpaka serikali mpya itakapoundwa. Wagombea demokrasia wana wasiwasi kuwa viongozi wa kijeshi hawana azma ya kuyakaribisha makundi yote ya upinzani katika mfumo mpya wa kisiasa nchini humo.

Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa na waakilishi wa sekta ya kiuchumi waliokuwa karibu sana na serikali ya Mubarak, wamepaswa kuwajibika. Waziri wa mambo ya ndani Anas al Fikki amewekwa katika kifungo cha nyumbani. Yeye anatuhumiwa kuhusika na rushwa. Hata baadhi ya wafanyabiashara hawana ruhusu kuondoka nchini na akaunti zao zimezuiliwa. Na katika jitahada ya kutuliza wasiwasi uliozuka kuhusu msimamo wa Misri kuelekea Israel, kufuatia matukio ya hivi karibuni, msemaji wa kijeshi Ismail Etman amesema:

"Mikataba yote ya kimkoa na kimataifa itaheshimiwa, ukiwemo pia mkataba wa amani pamoja na Israel."

Wakati huo huo, jeshi lililotuhumiwa na makundi ya haki za binadamu kuwa limewazuia na kuwatesa wanaharakati, wakati wa maandamano ya upinzani, sasa limeahidi kuwatafuta waandamanaji wote waliotoweka. Hiyo jana, wanaharakati wa Kimsri waliotumia mtandao kuongoza maandamano yao, kumng'oa madarakani Hosni Mubarak, walikutana na viongozi wa kijeshi kujadili mageuzi ya kidemokrasia. Wanaharakati wanane walikuwa na majadiliano pamoja na Jemadari Mahmud Hegazy na Jemadari Abdel Fattah, walio katika baraza kuu la kijeshi linalowakilishwa na majemadari 20.

Mkutano huo ni ishara kuwa jeshi linataka kuachana na mfumo wa serikali ya Mubarak, iliyokawia kutambua kuwa wanaharakati vijana ni kundi halali la upinzani. Baraza hilo la kijeshi limeahidi kufungua njia ya kuchagulia serikali ya kiraia na kujenga taifa huru la kidemokrasia.

Mwandishi: Ehl,Hans Michael/ZPR/P.Martin
Mpitiaji: Yusuf Saumu Ramadhani