1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wakamatwa kwa tuhuma za kuua waandamanaji

Saumu Mwasimba
11 Juni 2019

Hatua ya kuswekwa rumande wanajeshi kadhaa imechukuliwa na baraza la jeshi linaloongoza nchi wakati Marekani ikiwa imetangaza kumtuma mjumbe wake wa ngazi ya juu kwenda Khartoum.

https://p.dw.com/p/3KARU
Sudan | Protest | Militär in Khartoum
Picha: Reuters/U. Bektas

Wanajeshi kadhaa wanashikiliwa rumande kufuatia kuuwawa kwa watu chungunzima katika maandamano ya amani mjini Khartoum wiki iliyopita. 

Jumatatu usiku Marekani ilitangaza kwamba mjumbe wake wa ngazi ya juu kuhusu Afrika Tibor Nagy ataelekea Sudan kukutana na makundi ya upinzani pamoja na baraza la kijeshi linaloshikilia madaraka ya nchi kwa sasa.

Lakini ndani ya Sudan Kwenyewe baraza la kijeshi la mpito lilitowa taarifa hiyo jana usiku kupitia shirika la habari la taifa Suna likisema kuna ushahidi wa awali uliopatikana dhidi ya wanajeshi kadhaa  kuhusiana na kuuliwa kwa waandamanaji kiasi 100 na kujeruhiwa kwa wengine wasiopungua 500 wiki iliyopita.

Sudan Protest vor Militärhauptquartier in Khartum
Picha: picture-alliance/AP Photo

Wanajeshi hao imearifiwa kwasasa wanashikiliwa rumande mjini Khartoum. Baraza la kijeshi pia limesisitiza kwamba halitochelewesha hatua ya kuwawajibisha wote waliokutwa na hatia kwa mujibu wa taratibu na sheria.Mariam Al Mahdi naibu mwenyekiti wa chama cha Ummah kuhusu kitendo cha kuuliwa waandamanaji Juni tatu, anasema.

''Kilichotokea ni kitu kisichokubalika na kinachozua maswali mengi na tunakitizama kama njia ya kuvuruga mustakabali wa Sudan na umuhimu wa amani ambayo inahitajika kwa uthabiti,usawa na demokrasia nchini Sudan.''

Hali imeendelea kuwa ya wasiwasi na mashaka katika mji mkuu Khartoum ambapo kufikia jana iliarifiwa kwamba maduka mengi yalikuwa yamefungwa katika siku ya pili ya mgomo na maandamano ya nchi nzima yaliyoitishwa na makundi ya   upinzani.

Mohammed Salem ni miongoni mwa waandamanaji na mkaazi wa Khartoum anasema hakuna njia nyingine mbadala ya kulishinikiza jeshi isipokuwa kuendelea na harakati za maandamano.

Afrika | Protests im Sudan
Picha: picture-alliance/dpa/AA/M. Hjaj

''Bila shaka ni kwamba  harakati hizi za kuvunja sheria zinaiathiri nchi.Lakini ni kitu ambacho bado kinahitajika kuendelea kufanyika. Watu wamepata shida sana na ikiwa hawatofanya hivi basi harakati za mapinduzi zitakuwa zimepotea''

Juhudi za kuutafutia suluhisho mgogoro huo kati ya jeshi na makundi ya upinzani zilizofanywa na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed aliyekutana na pande zote wiki iliyopita bado hazijaonesha mafanikio yoyote.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Sekione Kitojo