1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi zaidi wahitajika Ujerumani

5 Desemba 2015

Kutokana na ushiriki wake katika utatuzi wa mizozo kadhaa inayoendelea ulimwenguni, jeshi la Ujerumani limesema idadi ya wanajeshi wake kwa wakati huu haitoshi na kwamba inahitaji wengine kuweza kuyatimiza majukumu yake.

https://p.dw.com/p/1HHvy
Wanajeshi wa Ujerumani katika mazoezi
Wanajeshi wa Ujerumani katika mazoeziPicha: picture-alliance/dpa/U.Baumgarten

Baada ya bunge la Ujerumani kuidhinisha kupelekwa kwa wanajeshi wa nchi hiyo kujiunga na mapambano dhidi ya wanamgambo wa Dola la Kiislamu nchini Syria, Jeshi la nchi hiyo, Bundeswehr, limesema linahitaji wanajeshi zaidi. Msemaji wa umoja wa jeshi hilo Andrea Wuestner ameliambia gazeti la Passauer Neue Presse, kwamba wanajeshi wapya kati ya 5,000 na 10,000 wanahitajika.

Msemaji huyo amesema mnamo miaka ya nyuma, idadi ya wanajeshi wa Ujerumani imepunguzwa kwa kiasi kikubwa, kwa sababu wakati huo hakuna aliyetarajia kuibuka kwa mizozo ya sasa.

Wuestner amesema kwamba mwaka 2011 wanasiasa hawakutarajia kwamba mwaka 2016 wangehitajika wanajeshi zaidi ya 20,000 wa kutumika katika shughuli za kijeshi za kila siku, na shughuli nyingine kama kuushughulikia mgogoro wa wakimbizi.

''Kwa sasa ujumbe wa kijeshi nchini Afghanistan umeongezewa muda, na tunahitajika pia kaskazini mwa Iraq, na nchini Mali,'' amesema msemaji huyo.

Hakuna ushirikiano na Assad

Siku ya Ijumaa (04.12.2015) bunge la Ujerumani, Bundestag liliridhia mpango wa kuwapeleka wanajeshi 1,200 nchini Syria kujiunga na operesheni dhidi ya wanamgambo wa IS.

Ijumaa, Bunge la Ujerumani, Bundestag liliidhinisha kupelekwa kwa wanajeshi wa Ujerumani na silaha kusaidia kulitokomeza kundi la IS.
Ijumaa, Bunge la Ujerumani, Bundestag liliidhinisha kupelekwa kwa wanajeshi wa Ujerumani na silaha kusaidia kulitokomeza kundi la IS.Picha: Reuters/F. Bimmer

Hata hivyo, mkurugenzi katika ofisi ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Peter Altmaier amesema kwamba wanajeshi hao wa Ujerumani hawatashirikiana na jeshi la serikali ya Rais wa Syria, Bashar al-Assad, kutokana na matendo ya jeshi hilo kuwashambulia raia kwa kutumia mabomu ya mapipa, hali ambayo amesema imechangia kuwafanya maelfu ya wasyria kukimbilia Ulaya.

Kuhusiana na kitisho cha wanamgambo hao wa IS, Rais wa Marekani Barack Obama amesema kundi hilo haliwezi kuichachafya nchi yake. Hayo ameyasema wakati ambapo inaendelea kudhihirika kwamba washambuliaji wawili waliouwa watu 14 kwenye hafla katika mji wa San Bernardino jimboni Calfornia, walifanya hivyo kutokana na ushawishi wa Dola la Kiislamu. Obama amesema watafanya ''uchunguzi wa kina'' kujua namna na sababu ya kutokea kwa mashambulizi hayo.

Obama aomba ushirikiano dhidi ya itikadi kali

Rais Barack Obama ambaye alikuwa akizungumzia suala la udhibiti katika umiliki wa bunduki nchini Marekani, amesema upo uwezekano kwamba washambuliaji hao walirubuniwa kwa itikadi kali za kiislamu kufanya kitendo hicho kiovu.

Rais wa Marekani Barack Obama
Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: picture-alliance/dpa/O. Douliery

Wote kwa pamoja, serikali, vyombo vya sheria, jamii na viongozi wa kidini, tunawajibika kushirikiana kuhakikisha kwamba watu hawawi wahanga wa itikadi hiyo ya chuki,'' amesema Rais huyo wa Marekani.

Washambuliaji hao, Syed Farrok mwenye umri wa miaka 28 ambaye ni mwislamu aliyezaliwa nchini Marekani, na mkewe Tashfeen Malik wa miaka 29 ambaye ni mpakistan, waliuawa na polisi baada ya shambulio hilo.

Wakati huo huo, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Laurent Fabius, amesema kwa sasa haamini kuwa ni lazima Rais wa Syria Bashar al-Assad aondoke madarakani kabla ya mchakato wa kisiasa kuanza, kutafuta suluhisho kwa mzozo wa Syria. Hata hivyo, Fabius amesema lazima kuwepo uhakikisho wa mustakabali wa nchi hiyo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae/afpe

Mhariri:Caro Robi