1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yaendelea kuzishambulia ngome za PKK

29 Julai 2015

Ndege za kivita za Uturuki zimefanya mashambulizi makali zaidi dhidi ya wanamgambo wa Kikurdi kaskazini mwa Iraq tangu operesheni ya mashambulizi ya anga ilipoanza wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/1G6nf
Syrien Türkische Luftangriffe auf die kurdische PKK
Picha: picture-alliance/AA

Hayo yamejiri saa chache baada ya Rais Tayyip Erdogan kusema kuwa mchakato wa amani umeshindikana.

Ndege aina ya F-16 ziliyapiga maeneo sita nchini Iraq na kurejea katika kambi ya jeshi la angani ya mkoa wa kusini mashariki wa Diyarbakir nchini Uturuki. Uturuki ilianza kuzilipua ngome za wanamgambo wa PKK kaskazini mwa Iraq Ijumaa iliyopita katika kile maafisa wa serikali walisema ilikua hatua ya kujibu msururu wa mauaji ya polisi na wanajeshi wa Uturuki yanayodaiwa kufanywa na kundi hilo la wanamgambo wa Kikurdi.

Hapo jana, ndege za kivita pia ziliyashambulia maeneo ya PKK katika mkoa wa kusini mashariki mwa Uturuki, Sirnak, unaopakanana Iraq baada ya kuwashambulia wanajeshi wa Uturuki.

Türkei Luftangriffe auf Kurden im Irak
Ndege ya kivita ya Uturuki aina ya F-16Picha: Reuters/M. Sezer

PKK imesema mashambulizi hayo ya kutokea angani, yaliyoanzishwa sambamba na mashambulizi ya Uturuki dhidi ya wapiganaji wa Dola la Kiislamu, IS nchini Syria, yanaufanya mchakato wa amani kutokuwa na maana yoyote. Lakini bado kundi hilo halijatangaza rasmi kujiondoa katika mazungumzo hayo.

Msemaji wa chama tawala Uturuki, AKP, Besir Atalay amesema jana kuwa mchakato wa amani kati ya Uturuki na wanamgambo wa Kikurdi unaweza kuendelea tu ikiwa “makundi ya kigaidi” yataweka chini silaha na kuondoka nchini humo.

Ofisi ya waziri mkuu imesema kuwa kufikia sasa jumla ya watu 1,302 wamekamatwa kote nchini humo katika mikoa 39 kufuatia misako iliyofanywa dhidi ya washukiwa wa IS, PKK na makundi mengine ya itikadi kali.

Bunge la Uturuki linatarajiwa kukutana baadaye leo katika kikao cha faragha, kujadili operesheni za kijeshi nchini Iraq na Syria, pamoja na wito wa Erdogan wa kuondoa amri ya kinga.

Erdogan alianzisha mazungumzo mwaka wa 2012 kujaribu kumaliza uasi wa PKK, unaofanywa kwa kiasi kikubwa katika eneo la kusini mashariki lenye wakaazi wengi wa Kikurdi, ambao umeuwa watu 40,000 tangu mwaka wa 1984. Mpango dhaifu wa kuweka chini silaha umekuwa ukitekelezwa tangu Machi 2013.

Washirika wa magharibi wamesema wanaitambua haki ya Uturuki kujilinda yenyewe lakini pia wameiomba nchi hiyo mwanachama wa NATO kutoua juhudi za kupatikana amani na kundi la PKK.

Wakati wakilichukulia kundi la PKK kuwa la kigaidi, serikali ya Marekani inategemea kwa kiasi kikubwa wapiganaji wa Kikurdi wa Syria katika vita vyake dhidi ya IS nchini Syria.

Mwandishi: Bruce Amani/REUTERS
Mhariri: Iddi Ssessanga