1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanamgambo wakipalestina washambulia Israel

26 Juni 2008

Israel ikiendelea kufunga mpaka wake na gaza

https://p.dw.com/p/ERZ4

Wanamgambo wakipalestina katika ukanda wa Gaza leo wamerusha tena maroketi dhidi ya eneo la kusini mwa Israel na kuyatia mashakani zaidi makubaliano ya kusitisha mapigano na Israel ambayo imeamua kufunga mipaka yake na eneo hilo la Gaza linalodhibitiwa na chama cha Hamas.

Kila upande sasa unamlaumu mwenzake kwa kukiuka makubaliano hayo yaliyosimamiwa na Misri wiki moja iliyopita. Wakati huohuo nchini Israel waziri mkuu Olmert amefanikiwa kuunusuru muungano wa chama chake usivunjike.

Tukianzia hali katika Gaza hakuna mtu aliyejeruhiwa kufuatia shambulio la roketi linalodaiwa kufanywa na kundi la wanamgambo wa al Aqsa lenye mafungamano na chama cha rais Mahmoud Abbas wa Palestina.

Shambulio hilo la leo limefuatia mashambulio mengine kadhaa yaliyofanywa jumanne na kundi la Islamic Jihad ya kulipiza kisasi dhidi ya uvamizi wa wanajeshi wa Israel ambao ulisababisha kuuwawa kamanda mmoja wa kundi hilo katika eneo la Palestina la Ukingo wa Magharibi linalokaliwa na Israel.Israel kwa upande wake ilisema uvamizi huo ulitekelezwa kwa lengo la kuvuruga mashambulio yaliyopangwa dhidi ya raia wake wanaoishi kwenye eneo hilo.

Mashambulio hayo ya roketi yameichochea Israel kufunga mipaka yake katika Gaza kwa siku mbili mfululizo kinyume na makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa wiki moja iliyopita.

Hata hivyo makubaliano hayo hayahusiani na eneo la Ukingo wa magharibi lakini makundi mengi ya wanamgambo yametishia kulipiza kisasi endapo Israel inaendelea na shughuli za kijeshi kwenye eneo la Ukingo wa Magharibi. Msemaji wa kundi la wanamgambo wa al Aqsa Abu Qusai amesema shambulio la roketi dhidi ya Israel limefanywa kulipiza kisasi ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano uliofanywa na Israel dhidi ya wapalestina walioko ukingo wa magharibi.

Israel kwa upande wake imesema hali hiyo inawafanya kuendelea kuufunga mipaka yake na ukanda wa Gaza bila ya kusema lini itafunguliwa.Si hayo tu lakini Israel imesema pia itaruhusu kufunguliwa mpaka wa Gaza na Misri kwa makubaliano na Hamas kwamba mwanajeshi wake Gilad Shalit aliyetekwa nyara miaka miwli iliyopita ataachiwa huru.Mjumbe wa Israel badae hii leo atakutana na mkuu wa usalama wa Misri Omar Suleiman kwa ajili ya kuzungumzia juhudi za kufikiwa makubaliano hayo ya kubadilishana mateka huyo Shalit na wafungwa wakipalestina walioko kwenye jela za Israel.

Hata hivyo msemaji wa chama cha Hamas Sami Abu Zuhri ameishutumu Israel kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano akisema kuendelea kufungwa mipaka ya Gaza kutayafanya makundi mengine kutoheshimu makubaliano hayo.

Aidha Hamas leo imefunga pia njia mbili za chini kwa chini za kupitishia silaha kutoka kusini mwa Gaza kuingia Misri.

Njia hizi kwa muda mrefu zimekuwa zikiwatia sana hofu waisrael.Wakati hayo yakiendelea nchini Israel muungano wa waziri mkuu Olmert umenusurika na mzozo mkubwa katika historia yake baada ya upinzani kuamua kuufutilia mbali muswaada unaotaka bunge livunjwe na uchaguzi wa mapema ufanyike.

Chama cha Labour kilikataa dakika za mwisho kuunga mkono muswada huo baada ya kufikia makubaliano na waziri mkuu Olmert kwamba chama chake cha Kadima kifanye uchaguzi ambao unaweza kumuondoa katika uongozi wa chama hicho kufikia septemba 25.

Mvutano katika muungano unaotawala Israel uliibuka mwezi uliopita baada ya polisi kuanzisha uchunguzi dhidi ya tuhuma za kashfa zinazomuandama waziri mkuu Olmert ambapo kiongozi wa chama cha Labour chama kikuu mshirika katika muungano huo Ehud Barak alimtaka waziri mkuu huyo ajiuzulu.

Olmert ambaye anakanusha tuhuma hizo alitishia kuwatimua serikali mawaziri wote wa chama hicho cha Labour ikiwa kundi lao litaungana na kiongozi wa upinzani Benjamin Netanyahu kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi wa mapema.

►◄