1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanamgambo wanne wa kipalestina wauwawa Gaza

25 Januari 2008
https://p.dw.com/p/Cxc6

Wanamgambo wanne wa kundi la Hamas wameuwawa leo kwenye mashambulio ya angani yaliyofanywa na jeshi la Israel mjini Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Msemaji wa jeshi la Israel amethibitisha mashambulio hayo dhidi ya motokaa zilizokuwa zimewabeba makamanda wa kundi la al Qassam ambalo ni kitengo cha kijeshi cha kundi la Hamas.

Mashambulio ya leo yamefanywa baada ya siku mbili ya machafuko katika Ukanda wa Gaza ambapo wanamgambo wa kundi la Hamas waliulipua ukuta katika mpaka wa kusini na kuwaruhusu maelfu ya wapalestina kuingia Misri.

Walinzi wa mpakani wa Misri leo wamesonga karibu na mpaka wa Ukanda wa Gaza kuwazuia wapalestina kuingia nchini Misri. Maafisa hao wanawaruhusu wapalestina wanaotaka kurejea Gaza baada ya kuitembelea Misri.

Israel imetangaza hali ya tahadhari katika mpaka wake wa kusini huku kukiwa na hofu kwamba wanamgambo wa Hamas huenda wakajaribu kuingia Israel kutoka Misri.

Umoja wa Ulaya umeitolea mwito Israel ivifungue vivuko vya mpakani kuingia Ukanda wa Gaza. Mratibu wa sera za kigeni wa umoja huo, Javier Solana, amezungumza kwa njia ya simu na rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas, kuhusu kuzorota kwa hali ya kibinadamu huko Gaza.