1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wananchi wa Msumbiji kupiga kura katika uchaguzi mkuu.

Halima Nyanza27 Oktoba 2009

Wananchi wa Msumbiji kesho wanapiga kura katika uchaguzi mkuu , kumchagua Rais na Bunge la nchi hiyo, huku chama tawala kikitarajia ushindi dhidi ya upinzani unaonesha kudhoofika kutokana na mpasuko uliopo.

https://p.dw.com/p/KGp2
Rais anayetetea nafasi yake katika uchaguzi wa kesho nchini Msumbiji, Armando Guebuza.Picha: picture alliance/landov

Chama kikuu cha upinzani nchini Msumbiji RENAMO na chama kilichojitenga kutoka katika chama hicho, cha Democratic Movement of Mozambique -MDM, tayari vinaonesha kuzigawa kura chache za upinzani na kukipa ushindi chama tawala cha FRELIMO, ambacho kimeongoza nchi hiyo toka kupatikana kwa uhuru wa Msumbiji mwaka 1975.

Rais anayetetea nafasi yake Armando Guebuza amepewa nafasi kubwa ya kuweza kuwashinda wapinzani wake, kiongozi wa chama cha RENAMO Afonso Dhlakama ambaye amewania nafasi hiyo kwa mara nne na kiongozi mwanzilishi wa chama cha MDM, Daviz Simango.

Wakati Frelimo wakiwa na uhakika wa ushindi, upinzani nchini humo unakabiliwa na changamoto kubwa kuweza kushinda uchaguzi huo.

Kiongozi wa Chama kikuu cha upinzani RENAMO Afonso Dhlakama, tayari amekosolewa na vyombo vya habari vya nchi hiyo kwa kusema kwamba ameshindwa kusimamia uendeshaji wa chama chake, hivyo RENAMO hakitafanya vizuri katika uchaguzi huo.

Katika kipindi cha miaka 15 tangu kuanzishwa kwa demokrasia ya vyama vingi nchini Msumbiji , RENAMO, ambacho ndio chama kikubwa cha upinzani hakujawahi kupata nafasi katika uchaguzi.

Licha ya baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya amani mwaka 1992 na kupisha njia ya kufanyika kwa uchaguzi wa kidemokrasia, chama hicho kimekuwa kikipigania kumaliza muonekano wake kama wapiganaji wa msituni.

Katika uchaguzi wa mwaka 2004, muungano wake ulipata asilimia 30 tu, ya kura zote zilizopigwa.

Akizungumzi kuhusu chama cha MDM, Joseph Hanlon, Mhariri wa Jarida moja la kisiasa nchini humo anasema chama hicho ni kipya na kwamba bado kinaonekana kuwa kinatokana na mpasuko uliokuwepo katika chama cha RENAMO.

Mhariri Joseph Hanlon anasema kwamba chama cha FRELIMO hakina hofu na MDM kwa mwaka huu, lakini inakihofia chama hicho katika kipindi cha miaka mitano ijayo

Wakati chama hicho cha MDM, kikipewa nafasi kubwa katika siku zijazo, Kiongozi wa MDM Daviz Simango ameikosoa tume ya uchaguzi akisema inatumiwa kuhujumu nafasi za chama chake katika uchaguzi wa bunge.

Bwana Simango ameruhusiwa kugombea Urais lakini chama chake kimeondolewa katika mikoa minane kati ya 13 kwenye uchaguzi wa bunge.

Simango amekishutumu chama tawala Frelimo kuwa kinaitumia tume kukihujumu chama chochote kinachotokeza kukipa Frelimo upinzani mkali.

Tume ya Uchaguzi nchini humo, inasema uamuzi wake umetokana na kasoro katika kuwasilisha fomu za wagombea, lakini Simango anakanusha madai hayo.

Chama cha upinzani cha MDC, kinamatumani kuwa kitapigiwa kura na wapiga kura ambao hawatavipigia kura vyama hivyo viwili vikubwa vya siasa vya Frelimo na Renamo.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp,ap)

Mhariri: Abdul-Rahman