1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pressefreiheit

Sekione Kitojo3 Mei 2010

Shirika la kutetea haki ya uhuru wa vyombo vya habari , waandishi wasio na mipaka lenye makao yake makuu mjini Paris , wamewataja wakandamizaji wakuu 40 wa uhuru wa vyombo vya habari duniani.

https://p.dw.com/p/ND7D
Waziri mkuu wa Urusi Vladimir Putin, kushoto ni mmoja kati ya viongozi waliotajwa kuendea kinyume uhuru wa vyombo vya habari.Picha: AP

Shirika la waandishi wasio na mipaka limetoa leo Jumatatu orodha duniani , ya hali ya uhuru wa vyombo vya habari. Licha ya kwamba hutolewa orodha mpya kila mwaka , lakini kila mara hupatikana wale wanaoendea kinyume haki za uhuru wa vyombo vya habari. Safari hii ni pamoja na wanasiasa, viongozi wa kidini na viongozi wa makundi ya wapiganaji.

Kila mtu ana haki ya kutoa mawazo yake, haki hii inajumuisha kuwa huru, uhuru wa kusema pamoja na kupata habari na fikra kutoka katika vyanzo vyovyote bila ya kuwekewa mipaka.

Makundi hayo yaliyotajwa kuwa yanakiuka uhuru wa kupashana habari, yana nguvu, ni hatari , hutumia nguvu na hawaguswi na sheria, limesema shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Paris la waandishi wasio na mipaka. Watu hawa wanaokandamiza uhuru wa vyombo vya habari wana nguvu za kukagua habari, kuwaweka kizuizini waandishi habari, kuwateka nyara, kuwatesa na katika hali mbaya kabisa hata kuwauwa waandishi habari.

Marais saba na viongozi kadha wa serikali wako katika orodha hii , ikiwa ni pamoja na rais wa China Hu Jintao, rais wa Iran Mahmoud Ahmedinejad, rais Paul Kagame wa Rwanda, Raul Castro wa Cuba na waziri mkuu wa Urusi Vladimir Putin.

Wengine wapya katika orodha hii ambayo hupitiwa upya kila mwaka ya wakandamizaji wa haki za uhuru wa habari ni pamoja na mkuu wa kundi la Taliban Mullar Omar.

Kiongozi huyo wa Taliban , ambaye ushawishi wake umesambaa hadi Pakistan pamoja na nchi nzima ya Afghanistan , anajiunga na orodha hiyo kwasababu kile kinachoitwa vita vitakatifu ambavyo anaviongoza pia hulenga vyombo vya habari, limesema shirika hilo.

Wahalifu hao wanaoongozwa na Mullar Omar huwatishia waandishi habari wa nchi hiyo ambao hawaandiki kuhusu mawazo yake, wakati mashambulio 40 ya Taliban yamelenga moja kwa moja waandishi habari pamoja na vyombo vya habari katika mwaka 2009.

Vitisho kwa waandishi habari vinaimarisha hali ya raia wa nchi hiyo kuelemea upande wa Taliban na kujenga hali ya ukosefu wa taarifa katika maeneo ya kusini na mashariki ya Afghanistan pamoja na eneo la magharibi nchini Pakistan.

Rais anayeelemea zaidi upande wa Urusi katika jimbo la Chechnya Ramzan Kadyrov pia ameongezwa katika orodha hii. Rais wa Yemen Ali Abdullah Saleh ameelezwa kuwa ni mkandamizaji mkubwa wa uhuru wa vyombo vya habari baada ya serikali yake mjini Sanaa kuunda mahakama maalum kwa makosa ya vyombo vya habari katika kile ambacho shirika la waandishi habari wasio na mipaka limesema ni juhudi za kupunguza taarifa za vita vichafu vinavyoendeshwa katika maeneo ya kaskazini na kusini mwa nchi hiyo.

Kila mwaka katika mwezi wa Oktoba shirika hilo la waandishi wasio na mipaka hutoa orodha ya hali ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, ambayo ni kielelezo kutoka mataifa 175 baada ya tathimini katika nchi hizo kuhusu uhuru wa habari. Kimsingi kuna orodha ya maswali 42, ambayo matawi ya shirika hilo katika nchi mbali mbali inapaswa kuyajibu. Hususan huhusisha wanasayansi, wanasheria, wanaharakati wa haki za binadamu pamoja na waandishi habari katika kila nchi inayohusika.

Mwandishi: Jeppesen,Helle/ZR/Sekione Kitojo

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman