1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaume wa Uganda wabuni mbinu za kukwepa majukumu yao

Mohammed Khelef
2 Desemba 2016

Huku dunia ikiadhimisha siku 16 za kuhamasisha jamii kupambana dhidi ya ukatili wa kijinsia, wanaume wakorofi nchini Uganda wamekuja na mbinu za kuwadhalilisha wanawake kimawazo kufidia marufuku ya kuwapiga.

https://p.dw.com/p/2TeEF
Afrika Uganda - Frauen tragen Wasserbehälter auf dem Kopf
Picha: Imago/Blickwinkel

Ingawa wanawake wa jamii ya Sabiny katika kata ya Korte wilayani Bukwo mashariki mwa Uganda kwenye miteremko ya Mlima Elgon huonesha furaha wakati wanapoimba, nyoyoni mwao wanasononeka kutokana na waume zao kukataa kuchangia katika kutunza familia.

Wengi wa wanawake hawa wanasema wanaume "wanakwepa majukumu yao ya kushughulikia mahitaji ya familia zao, wakidai kuwa ni kwa sababu sheria inawakataza kuwapiga wake zao."

"Wanaume zetu wameamua kutafuta visingizio," anasema Betty, ambaye ni mama ya nyumbani.

Kisingizio hiki wanachotoa wanaume kinatokana na kutafsiri kwao suala la usawa kwa kijinsia kwa namna hii ili wapate kuendeleza mfumo dume uliojikita katika utamaduni wa jamii nyingi za Afrika na kwingineko.

"Kinachosikitisha wanaume hawa hushinda siku kutwa kwenye ulevi na gumzo madukani au sokoni, baada ya kuuza mali ya familia ambayo imezalishwa na wanawake wakiwa na watoto wao," anaongeza Betty.

Wanaporudi nyumbani, baadhi ya wanaume huwa wamelewa chakari, lakini hutaraji kupewa chakula wasichojuwa kilipatikana vipi, anasema mwanamke mwengine aliyejitambulisha kwa jina la Lilian.

Hunger im Sahel Bildergalerie
Wakiwa wamewacha na waume zao wahudumie familia, wanawake wengi wa Sabiny hugeukia kuwa vibarua kwenye mashamba ya jirani.Picha: Fatoumata Diabate/Oxfam

Kwa kuwa akina baba kadhaa hawachangii kwenye mapato ya nyumbani, wanawake wanaelezea kuwa hiki ndicho chanzo cha umasikini kwenye ngazi za familia.

Katika juhudi zao za kukimu mahitaji ya familia zao, kwa hivyo, baadhi ya wanawake wameaumua kufanya vibarua kwenye mashamba ya majirani zao waweze kuziba pengo ambalo waume zao wamewaachia. "Lakini hata huko wao hunyanyaswa na waajiri wetu," anasema Betty.

Wakati huu mwezi Disemba ukiwadia, ambapo familia nyingi za imani ya Kikristo zinajiandaa kusherehekea sikukuu ya Krismasi, wanawake hawa wa kata ya Korte wamo katika mashaka makubwa, kwani bado ni jukumu lao kuona kwamba familia zao zinasherehekea siku hii maalum, na wanaume wamejitenga kando kama kwamba hawahusiki na dhima ya kifamilia.

Lakini kwa nini wanawake hawa wameamua kustahimili katika ndoa hizi ambazo kwa mtazamo wa wengine zina changamoto nyingi? "Kuishi katika ndoa hizi ni kutii amri na mapenzi ya Mungu", anajibu Betty, ambaye anakiri kwamba licha ya yote, anaendelea kumdekeza mumewe na kumtimizia haja zake zote.

Kuanzia tarehe 25 Novemba hadi 10 Disemba, Umoja wa Mataifa unaendesha kampeni ya kutokomeza ukatili wa kijinsia, lakini tabia za wanaume kukataa kuchangia katika kutunza familia zinastahili kushtumiwa na kuwahamasisha wabadili mwenendo huo.

Mwandishi: Lubega Emmanuel/DW Kampala
Mhariri: Mohammed Khelef