1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake Uganda sasa kushiriki kuandaa wosia wa mirathi

Admin.WagnerD7 Julai 2020

Maamuzi ya mahakama moja ya Uganda ya kumhusisha mke katika kuandaa wosia wa mirathi yamepokelewa kwa furaha na wanawake. Wanawake wengi huona haki zao zikikiukwa pale mume anapotoa mali zote kwa mtoto wa kiume.

https://p.dw.com/p/3etdD
Wasserknappheit in Afrika - Panorama
Picha: AP

Katika hali hii, mke ambaye anaweza kuwa hata mamake mrithi hujikuta hana mamlaka na umiliki kwa nyumba na mali waliyochuma pamoja na marehemu mumewe.

Kwa mujibu wa utamaduni wa kiafrika, mume ndiye mmiliki wa mali ya familia. Katika mazingira haya, pale anapoandika wosia na kumrithisha mwanawe mke wake hahusishwi hata kidogo. Aidha matarajio yangekuwa kwamba mrithi atatunza familia na mali ya marehemu. Lakini hii imekuwa kinyume kabisa kwani wengi hujikuta wametupwa nje hata ya nyumba waliochangia jasho lao kujenga.

Ni kwa ajili hii ndipo maamuzi ya mahakama ambayo sasa ni sharia rasmi yatalinda haki za wajane kuhusiana na suala la mirathi. Mbunge Rosette Mutambi ndiye aliwasilisha muswaada bungeni.

Maamuzi ya kesi hiyo yameleta furaha kubwa kwa wanawake. Wengi wao wamekuwa wakiishi katika maisha ya mashaka na ndiyo chanzo cha baadhi kununua na kuficha mali zao kama vile ardhi wasije wakapoteza kile walichokichuma.

Umiliki wa ardhi ni miongoni mwa mambo ambayo huleta mgogoro mkubwa katika familia hasa baada ya kifo cha mmoja kati ya wanandoa. Katika familia nyingi, mrithi ana mamlaka ya kuuza mali na kuwaacha mama na ndugu zake bila chochote. Lakini kufuatia sheria hii, hapana shaka kwamba wajane watapata haki zao. Hii ni kwa sababu utaratibu wa kuandika wosia utahitaji kumhusisha mke au mume moja kwa moja ili naye afahamu haki yake na mrithi ajue wajibu wake.

Togo Lome Frauen schälen Maniok
Wanawake barani Afrika wamekuwa wazalishaji wakubwaPicha: picture-alliance/robertharding/Godong

Sheria hii aidha inalinda haki za wanandoa wanapotalikiana kwani kila mmoja ana haki sawa. Shauri lililowasilishwa mahakamani mwaka 2000 ndilo limekuwa chanzo cha sheria hiyo kuibuka. Mlalamikaji katika kesi hiyo alikuwa bibi ambaye alikuwa akipigania haki zake dhidi ya mjukuu wake aliyemrithi babake mrithi wa mumewe.

Kulingana na jaji aliyetoa maamuzi, ni jambo la kawaida kwamba mume au mke akifa hata kama hakuacha wosia wa mirathi na walikuwa wanandoa halali basi aliyebaki anachukua umiliki wa mali yao.

Huku wanaharakati wakiendelea kusherehekea ushindi huo, mbunge Rosette Mutambi anawataka waangazie suala la kuhamasisha watu wote hasa wanawake kuhusu sheria hiyo mpya ambayo kwa baadhi haijaeleweka.

Lubega Emmanuel DW Kampala