1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake wa Afghanistan waandamana kutaka haki zao kulindwa

Amina Mjahid
2 Septemba 2021

Wanawake kadhaa wameandamana mbele ya ofisi ya gavana wa mkoa wa Herat Magharibi mwa Aghanistan, wakitaka serikali mpya izingatie haki zao baada ya Taliban kuchukua madaraka

https://p.dw.com/p/3zpsx
Afghanistan Herat | Protest Frauen
Picha: Mir Ahmad Firooz Mashoof/Anadolu Agency/picture alliance

Friba Kabrzani, mmoja ya waandaaji wa maandamano ya leo alhamisi, amesema wanawake wanapaswa kushirikishwa kisiasa katika serikali mpya ikiwemo kujumuishwa katika Baraza la Mawaziri na Baraza la wazee wa kikabila linalojulikana kama Loya Jirga.

Kabrzani amesema kwa miaka 20, wanawake wa Aghanistan wamejitolea kwa mengi kufikia walipo sasa, kwahiyo wanachotaka ni dunia kuwasikia na kuzinusuru haki zao. Amesema baadhi ya familia hazikukubali wanawake wao kushiriki katika maandamano hayo wakihofia usalama wao, kufuatia kundi la Taliba kuchukua udhibiti wa nchi katikati ya mwezi Agosti.

Maryam Ebrahim aliyeshiriki maandamano hayo amesema licha ya Taliban kutoa hotuba nzuri  kupitia televisheni bado kumekuwepo na ripoti za matumizi mabaya ya madaraka yanayofanywa hadharani.

"Tumewashuhudia wakiwapiga tena wanawake," alisema Maryam huku akiongeza kuwa wataendelea na maandamano yao hadi pale haki zao zitakapotambuliwa.

soma zaidi: Afrika Kusini yakataa kuwapokea wakimbizi wa Afghanistan

Maandamano hayo yanafanyika wakati Watawala  wa Kundi la Taliban wakitarajiwa kuitangaza serikali yao mpya. Kiongozi Mkuu wa kundi hilo Haibatullah Akhundzada, anatarajiwa kuchukua madaraka ya juu zaidi katika baraza jipya la uongozi huku rais wa nchi akiwa chini yake.

Uingereza: tunaweza kuzungumza na Taliban bila kuitambua serikali yao

UK Aussenminister Dominic Raab
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Dominic RaabPicha: Ashraf Shazly/Getty Images/AFP

Kwengineko Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Dominic Raab amesema- licha ya  taifa lake kutoitambua serikali ya Taliban hivi karibuni, kuna nafasi muhimu ya mazungumzo na watawala hao wapya wa Afghanistan.

Katika mkutano wa pamoja na waandishi habari, na mwenzake wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman al-Thani, Raab ameunga mkono majadiliano na kundi hilo ili kupima ahadi walizozitoa ikiwa ni pamoja na kulinda uhuru wa kusafiri kwa waafghanistan na raia wa kigeni, kuunda serikali inayoyashirikisha makundi yote ya kisiasa na muhimu ni kuzuwiya makundi ya kimataifa ya ugaidi  kutumia nchi hiyo kama ngome yao.

Taliban kutangaza serikali yake licha ya uchumi kuyumba Afghanistan

Raab amesema watalipima kundi hilo kutokana na kile wanachokifanya na sio kile wanachokisema. Kutambuliwa kwa kundi la Taliban ni muhimu ili kuliwezesha kufikia misaada ya miradi ya maendeleo na pia nafasi ya kukopa fedha kutoka taasisi za kimataifa za fedha.

Wakati huo huo waziri wa mambo ya kigeni wa Qatar Mohammad bin Abdulrahman Al Thani, amesema haijawa wazi ni lini uwanja wa ndege wa kabul utafapofunguliwa tena lakini wapo katika mazungumzo na Taliban kuhakikisha hilo linafanyika hivi karibuni. 

Operesheni katika uwanja huo zilisitishwa tangu katikati mwa Agosti wakati Taliban walipoudhibiti mji wa Kabul, lakini ndege za kijeshi ziliendelea kufanya kazi hadi Agosti 31 wakati wanajeshi wa kigeni walipoondoka nchini humo.

Chanzo: reuters,dpa