1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wangaalizi wa amani hatarini Syria

Admin.WagnerD16 Mei 2012

Waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria wameondolewa katika mji wa Khan Sheikhoun, kaskazini mwa nchi hiyo siku moja baada ya msafara wao kupigwa na kombora katika makabiliano kati ya vikosi vya serikali na waasi.

https://p.dw.com/p/14waU
Waangalizi wa amani wakikagua mabaki ya gari ya Sheikh Abdul-Aziz al-Hafi baada ya mlipuko katika kijiji cha Deir Al-Zour.
Waangalizi wa amani wakikagua mabaki ya gari ya Sheikh Abdul-Aziz al-Hafi baada ya mlipuko katika kijiji cha Deir Al-Zour.Picha: picture-alliance/dpa

Mashambulizi hayo ambayo yalikuja muda mfupi baada ya shahidi mmoja kusema kuwa majeshi ya serikali ya Syria yaliwauwa kwa risasi waombolezaji waliyokuwa kwenye msiba karibu na eneo la tukio yamezidi kuuweka mashakani mpango wa amani wa Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Koffi Annan.

Wanaharakati wamesema vurugu ziliendelea Jumatano ambapo vikosi vya serikali vilifyatua risasi hovyo katika maeneo ya jirani na Khan Shaikhoun. Mkuu wa Shirika la uangalizi wa haki za binadamu nchini humo, Rami Abdul Rahman, alisema mashambulio ya risasi yalifanya mazishi ya watu 20 waliouawa kwenye msiba huo kushindwa kufanyika.

Moja ya magari yaliyokuwa kwenye msafara wa waangalizi likiwa limeharibiwa na mlipuko wa bomu.
Moja ya magari yaliyokuwa kwenye msafara wa waangalizi likiwa limeharibiwa na mlipuko wa bomu.Picha: Reuters

Mauaji ya kimbari
Shirika hilo lilisema majeshi ya serikali yaliwachinja raia kumi na watano usiku wa kuamkia JUmatano katika kijiji kimoja kilichopo mkoani Homs. Rami aliliambia shirika la habari la AFP kuwa mauaji hayo yanastahili kuitwa ya kimbari. Kiongozi wa dini mwenye umri wa miaka 43 na baba wa watoto sita ambaye alikuwa kipenzi cha watu wa eneo hilo na mhimizaji wa umoja wa kitaifa alikuwa miongoni mwa watu waliochinjwa.

Umoja wa Mataifas ulisema waangalizi wake waliozingirwa katika mapigano hayo wakati wa mkutano na jeshi la waasi la Free Syria, walihifadhiwa na waasi na msemaji wa Koffi Annan, Ahmad Fawzi, alisema katika taarifa yake kuwa sita kati ya hao walipatiwa matibabu wakiwa mikononi mwa waasi. Zaidi ya waagalizi 200 tayari wako nchini Syria kusimamia makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yamekuwa yanakiukwa na pande zote tangu yaanze kutekelezwa Aprili 12.

Mwanajeshi wa jeshi la waasi akikimbia kujificha katika wilaya ya Jabb al-Jandali, mkoani Homs.
Mwanajeshi wa jeshi la waasi akikimbia kujificha katika wilaya ya Jabb al-Jandali, mkoani Homs.Picha: AP

Mripuko huu ni wa pili kuhusisha waangalizi hawa wa Umoja wa Mataifa baada ya bomu lililotegwa barabarani kuripuka wiki iliyopita sekunde chache tu baada ya msafara wa kiongozi wa waangalizi Meja Jenerali Robert Mood kupita, na kujeruhi wanajeshi waliyokuwa wanasindikiza msafara wake.

Iran yataka muda zaidi kutekeleza mpango wa amani
Lakini Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Ali Akbar Saleh amesema serikali ya Syria inahitaji kupewa muda zaidi kuweza kutekeleza mpango wa amani na kuomba mataifa yanayoizunguka Syria kusaidia katika hilo. Akbar ambaye hakutaja wazi mataifa gani, alikuwa akizilenga Saudi Arabia na Qatar ambazo zilionya siku ya Jumatatu kuwa mpango wa Anna ulikuwa unaelekea kushindwa.

Aliongeza kuwa serikali imechukua hatua katika kufanya mageuzi ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho ya Katiba na kuandaa uchaguzi tarehe 7 Mei ambao hata hivyo ulisusiwa na wapinzani.

Mgorogro wa Syria uliyodumu kwa miezi kumi na minne, umeshaua zaidi ya watu 12,000, wengi wao wakiwa raia wa kawaida kwa mujibu wa shirika la haki za binadamu la nchi hiyo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE\APE
Mhariri: Othman Miraji