1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapi watakwenda wafungwa wa Jela la Guantanamo?

Miraji Othman24 Desemba 2008

Jee wafungwa wa Ki-Uigur kutoja Gereza la Guantanamo watakuja Ujerumani?

https://p.dw.com/p/GMbU
Wafungwa katika gereza la Kimarekani la Guantanamo, CubaPicha: AP

Karibu watu wote wanataka gereza la Guantanamo lifungwe, na Rais mteule wa Marekani, Barack Obama, sio wa mwisho kati ya watu wanaotaka jambo hilo. Lakini nani atawapa hifadhi hao watu watakaoachwa huru kutoka gereza hilo? Hapa Ujerumani zingatio liko juu ya kundi la wafungwa wa kabila la Uigur ambao ni Waislamu wa kutoka Uchina.

Rais Barack Obama anataka gereza la Guantanamo lililoko Cuba lifungwe, lakini anahitaji mshirika. Na mshirika huyo ni serekali ambazo zitakuwa tayari kuwachukuwa wafungwa wa zamani wa jela hilo watakaoachwa huru, na ambao wanatishiwa kuteswa katika nchi zao pindi watarejea huko. Hadi sasa hapa Ulaya nchi ambazo zimesema zitakuwa tayari, kimsingi, kuwachukuwa wafungwa hao wa zamani wa Guantanamo ni Ureno na Ujerumani.

Mjini Berlin kunazingatiwa kukichukuwa kikundi cha Wa-Uigur 17, kabila dogo linaloishi katika Mkoa wa Xinjiang, mkoa ulio na utawala wa ndani Magharibi ya Uchina. Serekali ya Uchina inataka watu hao warudishwe Peking, ikitoa sababu kwamba wao ni wanachama wa jumuiya ya kigaidi. Marekani imelikataa ombi hilo la Uchina. Hifadhi watakaoipata hapa Ujerumani itawalinda wafungwa hao wa zamani kusumbuliwa na wakuu wa Uchina, huenda wataepukana na kuteswa na kupewa adhabu ya kifo. Mmoja wao ni Adel Noori.

Kwa miaka sita sasa, Adel Noori, mwenye umri wa miaka 28, anavaa nguo ilio na nambari 584 katika gereza hilo lililoko Cuba. Chumba chake ni kama tundu la vyuma, halina mwangaza. Mwaka 2002, miezi michache baada ya kuondoshwa madarakani Wataliban huko Afghanistan, alikamatwa, akishukiwa kuusaidia ugaidi wa kimataifa.

Wakuu wa kijeshi wa Marekani wanaamini kwamba Adel Noori ni mwanachama wa vuguvugu la Kiislamu la Mashariki ya Turkestan, ETIM, jumuiya ambayo imeorodheshwa pia na Marekani na Umoja wa Mataifa kuwa ya kigaidi. Kwa mujibu wa serekali ya Uchina, jumuiya hiyo ya ETIM inapigania kwa kutumia nguvu za kigaidi uhuru wa jimbo la Xinjiang huko Magharibi ya Uchina. Chama hicho cha ETIM kinaliita eneo hilo la Uchina ambalo liko katika mpaka na India, Pakistan na Afghanistan kuwa ni Turkestan ya Mashariki. Kutokana na tarakimu za karibuni za kuwahesabu watu huko Uchina, wanaishi Wa-Uigur milioni saba katika mkoa huo, wengi wao ni Waislamu wa madhehebu ya Sunni.

Wa-Uigur wengi, kama vile Adel Noori na wenzake kumi na sita walioteseka huko Guantanamo, wanahisi wanakandamizwa kisiasa na kidini huko kwao na pia wanaonewa, kiuchumi. Kwa mujibu wa jumiiya ya Ujerumani inayoshughulikia jamii za watu wanaotishiwa hapa duniani, tangu mwaka 1998 si chini ya Wa-Uigur 700 wamenyongwa kutokana na sababu za kisiasa. Maandamano yao huko Uchina hukandamizwa kikatili. Ndio maana Wa-Uigur wengi wanaamuwa kuikimbia nchi yao na kuanza maisha mepya katika nchi za jirani, uamuzi ambao wengi wao unawapeleka katika hali duni. Huko Afghanistan wanakamatwa na kichwa cha kila mmoja wao huuzwa hadi dola 5,000 kwa wamarekani; hivyo ndivyo wanavosema mawakili wa wafungwa hao wa Guantanamo.

Serekali ya Marekani imeachilia mbali mashtaka yake ya ugaidi dhidi ya Wa-Uigur hao kumi na saba walio na umri baina ya miaka 28 na 44 baada ya kutolewa yale malalamiko mbele ya mahakama huko Washington. Lakini kuachiliwa huru watu hao kumeshindwa kufanyika hadi sasa, kwa vile watu hao wameshindwa kupata nchi itakayokuwa tayari kuwachukuwa. Mwaka 2006, Wa-Uigur watano walikwenda Albania, lakini huko hawajakuta jamii ya Wa-Uigur. Ni wachache walioweza kwenda katika nchi za Umoja wa Ulaya, hadi Sweden.