1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiga kura nchini Iran watoa onyo kwa rais Ahmedinejad.

S.Kitojo18 Desemba 2006

Wapigakura wa Iran Jumapili iliyopita walitoa onyo kwa rais Mahmoud Ahmedinejad katika uchaguzi ambao umetikisa hali ya kisiasa kabla ya uchaguzi wa bunge katika muda wa miaka miwili ijayo. Sekione Kitojo anatathmini hali ya uchaguzi huo wa mabaraza ya miji nchini Iran.

https://p.dw.com/p/CBHt

Washirika wa rais mahmoud Ahmedinejad , ambaye alichaguliwa kuwa rais mwaka mmoja uliopita katika wimbi la kuungwa mkono na wengi, ameshindwa kuleta matumaini kwa ushindi katika chaguzi za serikali za mitaa ama baraza la wataalamu wa kidini.

Wapigakura wameonyesha ishara ya tahadhari kwa rais Ahmedinejad, amesema mchambuzi mhafidhina Amir Mohebian. Ni ishara wazi kabisa kwa Ahmedinejad. Umaarufu wa serikali unapungua , amesema Mohammed Atrianfar, mwanamageuzi ambaye alikuwa muasisi wa gazeti ambalo limepigwa marufuku hivi sasa la Shargh.

Wakati kura hizo ni vigumu kugundua kuwa ni kura ya maoni kuhusu umarufu binafsi wa rais Ahmedinejad, matokeo hadi sasa yanaonyesha kuwa serikali haijapata uungwaji mkono wa wazi katika wakati huu ambapo kuna idadi kubwa ya watu wasiokuwa na kazi pamoja na mfumuko wa bei unaondelea.

Ayatoullah amabye anaonekana kuwa ni mfano mkubwa wa kidini kwa Ahmedinejad , Mohammad Mesbah Taghi Yazdi, alikuwa bado yuko nyuma ya Akbar Hashemi Rafsanjani ambaye ni mwenye msimamo wa kati katika uchaguzi wa baraza la wataalamu.

Wakati huo huo , matokeo ya mwanzo yanaonyesha kuwa mabaraza ya miji katika miji mikubwa kama Tehran na Isfahan yatakuwa na utawala wa pamoja kati ya wahafidhina asilia ambao wanamuunga mkono Ahmedinejad na wanamageuzi pamoja na wahafidhina wa mrengo wa kati.

Somo kubwa katika uchaguzi hu uni kushindwa kwa marafiki wa Ahmedinejad na ushindi kwa wahafidhina wenye msimamo wa kati, Atrianfar amesema.

Ukweli kwamba Rafsanjani amepata kura nyingi zaidi kuliko Mesbah Yazdi ni ujumbe maalum wa wazi kisiasa. Matokeo hayo yanaonyesha wapigakura wamejifunza somo la siku za nyuma na wameona kuwa wanahitaji kurejesha uwiano katika medani ya kisiasa na kuunga mkono zaidi viongozi wenye msimamo wa kati.

Wadadisi wa mambo wanasema kuwa moja kati ya sehemu zinazofurahisha katika uchaguzi huo ni mgawanyiko wa makundi ya kihafidhina kati ya wale wenye imani kali wanaomuunga mkono Ahmedinejad na na wale ambao wana mtazamo wa kati zaidi.

Mgawanyiko huu ulizidishwa na kugombea kwa Mesbah Yazdi katika nafasi ya kuingia katika baraza la wataalamu katika orodha amabyo haikujumuisha majina ya Rafsanjani ama yeyote kati ya washirika wake.

Wakati huo huo washirika wa Rafsanjani ambaye ni mwenye ubavu katika siasa za Iran ambaye pia aliwaweka karibu wahafidhina na wenye msimamo wa kati katika miaka ya hivi karibuni , walijiunga pamoja na wanamageuzi kuwania viti vya baraza la mji wa Tehran kwa tikiti ya pamoja ya wale wanaolenga msimamo wa kati.

Uchaguzi huu umeonyesha kuwa wapiga kura bado wana imani na kambi ya wahafidhina , ambayo ni pamoja na wahafidhina wenye msimamo wa kati na waungaji mkono wa rais Ahmedinejad, amesema Mohebian.

Lakini wanapaswa kuweka kando tofauti zao katika kujitayarisha na uchaguzi ujao wa bunge mwaka 2008. Ama sivyo , hali itakuwa nzuri zaidi kwa wanamageuzi.

Maafisa wamesifu idadi kubwa ya watu waliojitokeza kupiga kura ambapo asilimia 60 ya wapigakura wamejitokeza na kuweka mtazamo mzuri wa watu wachache waliojitokeza katika chaguzi za hapo awali.