1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiga kura wa Burma wateremka vituoni kuwachagua wabunge

Oumilkher Hamidou7 Novemba 2010

Rais Barack Obama wa Marekani awataka watalawa wa kijeshi wamuachie huru mwanasiasa wa upande wa upinzani Aung San Suu Kyi

https://p.dw.com/p/Q0t9
Picha ya kiongozi wa upinzani Aung San Suu Kyi anaetumikia kifungo cha nyumbaniPicha: AP

Wapiga kura milioni 30 wa Burma wameteremka vituoni hii leo kulichaguwa bunge na mabaraza ya mikoa.Hii ni mara ya kwanza kwa uchaguzi kama huo kuruhusiwa na utawala wa kijeshi tangu zaidi ya miaka 20 iliyopita.Watawala wa kijeshi mjini Rangun wanawaruhusu wapiga kura katika nchi hiyo masikini ya Asia wayachague mabaraza mawili ya bunge na mabunge 14 ya mikoa.Hata hivyo wamejiwekea haki ya kuwateuwa robo moja ya wawakilishi wa taasisi hizo.

Mwanasiasa mashuhuri wa upande wa upinzani,mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel, bibi Aung San Suu Kyi anaetumikia kifungo cha nyumbani,ametoa mwito wa kususiwa uchaguzi huo.Chama chake,NLD kimepigwa marufuku.

Rais Barack Obama wa Marekani akiwa ziarani barani Asia amewataka viongozi wa kijeshi wa Burma wamuachie huru Aung San Suu Kyi.Waziri wake wa mambo ya nchi za nje Hillary Clinton amesema uchaguzi huo wa bunge unatoa sura halisi ya jinsi wanajeshi wanavyotumia vibaya madaraka.

Burma imekuwa ikitawaliwa na wanajeshi tangu mwaka 1962 na wameibadilisha jina ,na kuiita badala yake Myanmar.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/afp,reuters,dpa

Mpitiaji:Mohamed Dahman