1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapiganaji wa IS wafurushwa Aleppo

Sylvia Mwehozi8 Juni 2016

Vikosi vya upinzani nchini Syria vinavyoungwa mkono na ndege za kivita za Marekani vimeuzingira mji wa Marea, kaskazini mwa Mkoa wa Aleppo na kuwafurusha wapiganaji wa kundi la IS karibu na mpaka na Uturuki.

https://p.dw.com/p/1J2Qf
Syrien Kämpfe zwischen IS und Rebellen bei Allepo
Picha: Getty Images/AFP/Z. Al-Rifa

Vikosi vya upinzani nchini Syria vinavyoungwa mkono na ndege za kivita za Marekani vimeuzingira mji wa Marea, kaskazini mwa Mkoa wa Aleppo na kuwafurusha wapiganaji wa kundi la dola la kiislamu IS waliokuwa wakidhibiti eneo hilo muhimu karibu na mpaka na Uturuki. Wakati huo huo mawaziri wa ulinzi wa Syria, Iran na Urusi wanakutana mjini Tehran kwa mazungumzo juu ya hatua zaidi za kupambana na makundi ya wapiganaji.

Kwa mujibu wa kundi la uangalizi wa haki za binadamu la nchini Syria, mji wa Marea ulikuwa mikononi mwa wapiganaji wa IS kabla ya kufurushwa na vikosi vya upinzani.

Makundi ya wapiganaji yameuzingira mji huo baada ya kufanya shambulizi la kushutukiza dhidi ya IS baada ya kutoa taarifa kuwa wanaunganisha nguvu. Wamekitwaa kijiji cha Kafr Kalbin katika barabara inayounganisha Marea na Azaz, kilometa 20 kutoka kaskazini magharibi, taarifa hizo ni kwa mujibu wa kundi la uangalizi wa haki za binadamu.

Mkuu wa kundi la uangalizi wa haki za binadamu Rami Abdel Rahman ameliambia shirika la habari la DPA kuwa mji huo umezingirwa.

Mwezi Mei, IS iliuvamia mji huo wa Marea na kukata mawasiliano na mpaka wake na Uturuki.

Eneo la kaskazini mwa Aleppo nalo lilikata mawasiliano na kusini mwa Aleppo mwezi Februari na vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono na majeshi ya angani ya Urusi. Mapigano hayo yamesababisha maelfu ya raia kukwama katika mji wa Marea.

Mazungumzo Tehran

Wakati huohuo Waziri wa ulinzi wa Syria Fahd Jassem al-Freji atakutana na mawaziri wenzake wa Iran na Urusi siku ya Alhamisi. Urusi imetuma ndege za kivita na vikosi maalumu katika kuunga mkono utawala wa rais Bashar al-Assad wakati ambapo Iran ikipeleka washauri wa kijeshi na vifaa kwa wanamgambo wanaoiunga mkono serikali ya nchi hiyo.

Mojawapo ya jengo lililoharibiwa mjini Marea,Allepo.
Mojawapo ya jengo lililoharibiwa mjini Marea,Allepo.Picha: Getty Images/AFP/Z. Al-Rifa

Ziara ya waziri huyo wa ulinzi mjini Tehran, inakuja wakati ambao utawala wa Assad ukipiga hatua katika kampeni yake ya kupambana na IS na makundi mengine ya waasi mjini Aleppo.

Waziri mwenzake wa Urusi, Sergei Shoigu atahudhuria mkutano huo baada ya nchi yake kuahidi hatua zaidi za kuongeza mashambulizi ya angani dhidi ya waasi nje na ndani ya mji wa Aleppo, akishutumu upande wa waasi kwa kushindwa kutekeleza makubaliano ya mwezi februari ya kusitisha mapigano na kukata mafungamano na kundi la Al-Nusra lililo na mafungamano na Al-Qaeda.

Mazungumzo hayo ya mawaziri wa ulinzi yanakuja baada ya mwaliko wa mkuu wa majeshi wa Iran Hossein Dehghan.

Tehran imekuwa ikitoa msaada wa vifaa na fedha kwa serikali ya Syria tangu kuibuke uasi dhidi ya Bashar al-Assad miaka mitano iliyopita.

Mwandishi:Sylvia Mwehozi/DPA/AFP

Mhariri: Yusuf Saumu