1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani waitisha maandamano mapya Senegal

20 Februari 2012

Upinzani nchini Senegal umeitisha maandamano mapya leo (20-02-2012), wito unaoonekana kuchochea ghasia zaidi, siku sita kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu, ambapo Rais Abdoulaye Wade, atashiriki.

https://p.dw.com/p/1469g
Rais wa Senegal Abdoulaye Wade
Rais wa Senegal Abdoulaye WadePicha: dapd

Wakati zikiwa zimesalia siku sita kabla ya zoezi la uchaguzi mkuu, hofu ya kutokea machafuko zaidi inazidi kupanda, katika koloni hilo la zamani la Ufaransa, ambalo halijawahi kushuhudia vita wala mapinduzi ya kijeshi.

Tangu vurugu za kisiasa zianze mwishoni mwa mwezi uliopita, watu sita wamekwishapoteza maisha, katika makabiliano ya askari wa kutuliza ghasia na waandamanaji wanaompinga Wade, kushiriki katika kinyang´anyiro cha urais.

Vuguvugu la Mapinduzi ya tarehe 23 Juni, (M23), limepanga kuendelea kumshinikiza Wade, mwenye umri wa miaka 85, kuondoka madarakani, kabla ya Jumapili, siku ambayo Wasenegal watamchagua rais wanayemtaka.

Machafuko mjini Dakar
Machafuko mjini DakarPicha: picture-alliance/dpa

Mratibu wa M 23, Alione Tine amesema wamepanga maandamano hayo kuanza saa 15:00, tisa alasiri kwa saa za kimataifa, katika Uwanja wa Uhuru, katika mji mkuu, Dakar.

Uwanja huo uliofunikwa na majani, katika eneo la Plateau, uko jirani kabisa na ikulu ya Rais, na polisi wanashika doria kwa siku kadhaa sasa.

Akielezea ghasia za Ijumaa zilizosababisha watu kadhaa kujeruhiwa na kuuwawa, kiongozi mmoja wa Kiislam, Abdoul Aziz Ndoye; ameliambia Shirika la Habari la (APS), kuwa polisi walimpiga mpaka kumuua kijana mmoja ambaye alikuwa amekwenda dukani kununua mkate, katika mji wa Rufisque.

Polisi hao walikuwa wakifyatua hovyo risasi za mipira na kuwarushia raia gesi ya kutoa machozi, bila kujali ni nani aliyekuwa akishiriki maandamano hayo, katika miji mbalimbali ya Senegal.

Kutokana na matumizi hayo ya nguvu kubwa ya polisi dhidi ya wananchi, Waziri wa Ndani wa Senegal, Ousmane Ngom, aliomba radhi kwa kitendo hicho cha polisi, na kuwasihi wanasiasa kuendesha mikutano yao, mbali na maendeo ya misikiti.

Mwaka 2000, Wade aliingia madarakani baada ya kukishinda Chama cha Kisoshalisti, na sasa anapingwa vikali na wapiga kura wake, wanaolalamika kupanda kwa bei za vyakula, mgao mkali wa umeme, na nia yake ya kuendelea kuwatawala, uamuzi unaoonekana kumwandaa mwanae Karim Wade, kurithi kiti cha urais.

Marekani na Ufaransa wanapinga hatua ya Wade kugombea tena
Marekani na Ufaransa wanapinga hatua ya Wade kugombea tenaPicha: DW

Iwapo atachaguliwa, Wade ameahidi kujenga vyuo vikuu, barabara, viwanja vya ndege na kuanzisha miradi mikubwa ya kilimo nchini kote.

Senegal imeandikisha takriban wapiga kura milioni tano, na wagombea urais 13, wakiwemo waliokuwa mawaziri wakuu watatu.

Mwandishi: Pendo Paul\AFP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman