1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Compaore atuhumiwa kumuuwa Thomas Sankara

22 Desemba 2015

Korti ya kijeshi nchini Burkina faso imeamuru akamatwe rais wa zamani Blaise Compaoré,kuhusiana na madai ya kuuliwa mtangulizi wakeThomas Sankara,miaka 30 iliyopita.

https://p.dw.com/p/1HRZB
Rais wa Zamani wa Burkina faso,aliyeuliwa Thomas SankaraPicha: picture-alliance/dpa/AFP

Mauwaji ya kiongozi huyo aliyekuwa na haiba,mwaka 1987 ni mojawapo ya mauwaji ya kiajabu ajabu yaliyolikumba bara la Afrika baada ya uhuru na serikali ya mpito ya Burkina faso imepania kujua nani walihusika.

Mabaki ya mwili unaosemekana ni wa Thomas Sankara yalifukuliwa mapema mwaka huu na uchunguzi kuonyesha mwili huo umejaa risasi na kwa namna hiyo kuzidisha dhana kwamba aliuliwa kufuatia mapinduzi ya mwaka 1987 yaliyomleta madarakani Blaise Compaore.

Compaore binafsi alitimuliwa madarakani october mwaka jana na umati wa wananchi waliokuwa wakipinga kubadilishwa katiba ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi ili kumruhusu aendelee kuitawala nchi hiyo baada ya miaka 27 madarakani .Alikimbilia nchi jirani ya Côte d'Ivoire anakofikiriwa kupiga maskani yake.

Serikali ya Côte d'Ivoire haikuarifiwa

"Nnathibitisha jaji anaesimamia uchunguzi ametoa waranti wa kimataifa dhidi ya rais wa zamani Blaise Compaore" amesema Prosper Farama,wakili wa familia ya Sankara.Anasema Compaore anatuhumiwa miongoni mwa mengineyo kuhusika na mauwaji na kusaidia kundaa mauwaji.

Burkina Faso Ex-Präsident Compaore Archiv 2011
Muimla wa Zamani wa Burkina faso Blaise CompaoréPicha: picture alliance/AP Photo/R. Blackwell

Duru nyengine mbili za mahakama ambazo hazikutaka zitajwe,zimethibitisha waranti huo wanaosema umetolewa decemba nne iliyopita.Msemaji wa serikali hakuweza kupatikana kuthibitisha habari hizo.

Msemaji wa serikali ya Côte d'Ivoire amesema serikali yake haikuarifiwa.

Madai dhidi ya Compaore ni hatua muhimu mbele katika kesi hiyo katika wakati ambapo viongozi wa kipindi cha mpito wanajiandaa kumkabidhi hatamu za uongozi waziri mkuu wa zamani Roch Marc Kabore,mshindi wa uchaguzi wa rais wa Novemba iliyopita.

Uchunguzi wa vinasibu haukuleta matokeo yaliyotarajiwa

Thomas Sankara aliingia madarakani kufuatia mapinduzi ya kijeshi mwaka 1983 na kufuata nadharia ya Marx pamoja na ujamaa wa kiafrika-nadharia iliyompatia jina la "Che Guevara wa Afrika."Wasomi wengi wa Afrika wanamwangalia Thomas Sankara kuwa ni mwanasiasa aliyekuwa akiona mbali.

Burkina Faso Erinnerung an Präsident Thomas Sankara
Waburkinabé wanakumbuka siku aliyouliwa Thomas SankaraPicha: Getty Images/A. Ouoba

Wakili mwengine wa familia ya Sankara amesema tume ya wachunguzi wa kifaransa wameshindwa kutathmini vinasibu vya mabaki ya mwili unaosemekana kuwa ni wa kiongozi huyo aliyeuliwa.Familia ya Sankara wamepewa muda wa wiki mbili zaidi kupata maoni ya tume nyengine ya wataalam.

Watuhumiwa kumi wengine wanakabiliwa na kesi ya kuhusika na kuuliwa Sankara.Watuhumiwa hao ni pamoja na jenerali Gilbert Diendere aliyeongoza njama ya mapinduzi iliyoshindwa septemba mwaka huu.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AP

Mhariri:Yusuf Saumu