1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON: Bush apinga kuondosha vikosi Irak

13 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBj5

Baraza la Wawakilishi la Marekani,limepitisha mswada wa sheria unaotoa wito wa kuondosha baadhi kubwa ya vikosi vya Marekani kutoka Iraq,kuanzia kipindi cha siku 120 zijazo na hatua hiyo ikamilishwe ifikapo tarehe mosi Aprili.Mswada huo umepitishwa kwa kura 223 dhidi ya 201 zilizopinga.Wakati wa mdahalo,viongozi wa chama cha Demokratik walisema,sera za vita za Bush zimeshindwa na sasa ni wakati wa kuchukua hatua tofauti.

Lakini Rais George W.Bush angali akisisitiza kuwa vita vya Irak vinaweza kushindwa na amepuuza mito ya kubadili mkakati wa vita hivyo.Amesema, kuondosha vikosi ni kusalimisha hatima ya Irak mikononi mwa Al-Qaeda.Akaongezea kwamba kutokana na hatua zilizochukuliwa,kundi la Al-Qaeda hii leo limekuwa dhaifu kuliko vile ambavyo lingekuwa.

Lakini hoja zake zinapingwa na seneta wa chama cha Demokratik,Dick Durbin aliesema:

“Yuko mbali na ukweli wa vita vya Irak.Yuko mbali na umma wa Marekani.Tathmini ya ripoti tuliyoipata haitupi matumaini makubwa.“

Bush lakini amekwishasema kuwa hatotia saini mswada wowote utakaopanga tarehe ya kuondosha vikosi vya Marekani.