1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON: Maelfu wadai kurudishwa wanajeshi kutoka Iraq

28 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCXE

Mjini Washington Marekani makumi ya maelfu ya watu wanaopinga vita wamendamana kudai kurudishwa nyumbani kwa wanajeshi wa Marekani walioko nchini Iraq.

Mavetarani wa vita wa Iraq,jamaa za wanajeshi wa Marekani waliouwawa na wale ambao wanaendelea kutumikia jeshi nchini Iraq wameungana na wabunge na wanaharakati wa amani katika maandamano hayo.

Mcheza sinema na mwanaharakati mashuhuri wa vita dhidi ya Vietnam Jane Fonda ameueleza umati kwamba kunyamaza kimya sio tena chaguo na kwamba hawajajifunza kutokana na vita vya Vietnam.Baadhi ya waandamanaji wamebeba mabango yenye kutaka kuzuiliwa kutolewa kwa fedha zaidi kwa ajili ya vita vya Iraq na kukomeshwa kwa mauaji nchini humo.

Maandamano hayo yanakuja siku mbili baada ya kamati ya Masuala ya Kigeni ya baraza la senate la bunge la Marekani kuukataa mpango wa Rais George W. Bush wa Marekani kuongeza wanajeshi 21,000 wa ziada nchini Iraq.

Tokea uvamizi uliongozwa na Marekani nchini Iraq hapo mwaka 2003 maelfu kwa maelfu ya wananchi wa Iraq wamepoteza maisha yao na zaidi ya wanajeshi 3,000 wa Marekani wameuwawa.

Katika kipindi cha siku tatu zilizopita wanajeshi saba wa Marekani wameuwawa nchini Iraq kutokana na mashambulizi ya mabomu yaliotegwa barabarani na waasi.