1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON : Merkel ajadili Mashariki ya Kati na Bush

5 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCdF

Rais George W.Bush wa Marekani na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani hapo jana wameahidi kushirikiana kwa karibu katika kujaribu kutatuwa mzozo uliodumu kwa muda mrefu kati ya Israel na Wapalestina.

Viongozi hao wawili wamejadili mzozo huo wa Mashariki ya Kati wakiwa kwenye Ikulu ya Marekani pia wamezungumzia mpango wa nuklea wa Iran,mzozo wa Afghanistan na Iraq pamoja na sera za níshati na biashara.

Bush amesema amekubaliana na Merkel juu ya haja ya kuitisha mkutano wa kundi la pande nne linalojumuisha Umoja wa Ulaya,Umoja wa Mataifa,Urusi na Marekani lililoundwa kutayarisha kile kinachojulikana kama ramani ya amani kwa Waisraeli na Wapalestina.

Katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari Bush pia amesema atatangaza sera yake mpya kwa Iraq wiki ijayo ambapo Merkel amesema kisiasa watafanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba kuna maendelo mazuri nchini Iraq ambapo wananchi watakuwa hawana haja tena ya kuwa na hofu na usalama wao.

Katika suala la mzozo wa Mashariki ya Kati Merkel amesema angependelea Umoja wa Ulaya kuwa na sauti moja ambayo ni ile ile ya suluhisho wa kuwepo kwa mataifa mawili Israel na Palestina na kwa Wapalestina kuitambuwa Israel.

Ujerumani hivi sasa inashikilia nyadhifa zote mbili za Urais wa Umoja wa Ulaya na Kundi la Mataifa Manane yenye Maendeleo Makubwa ya Viwanda.