1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON: Musharraf ahimizwa na Bush kuitisha uchaguzi

8 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/C794

Rais wa Marekani George W.Bush amezungumza kwa simu na Rais wa Pakistan,Jemadari Pervez Musharraf na amemuhimiza kuondosha haraka amri ya hali ya hatari na kufanya uchaguzi kama ilivyopangwa.Bush alipozungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari alisema:

"Ujumbe niliompa Musharraf ni kuwa uchaguzi ufanywe haraka na anapswa kuacha madaraka yake ya kijeshi.Hawezi kuwa rais na mkuu wa majeshi wakati mmoja.Azma ni ile ile kama nchini Burma yaani kuendeleza demokrasia nchini Pakistan."

Kwa upande mwingine,kiongozi wa upinzani Benazir Bhutto ambae pia ni waziri mkuu wa zamani wa Pakistan,anatazamia kuwa na mkutano wa hadhara siku ya Ijumaa,mjini Rawalpindi licha ya kuwa mikutano ya aina hiyo imepigwa marufuku.Kiongozi huyo wa upinzani vile vile ametishia kuandamana na wafuasi wake,ikiwa Musharraf hatorejesha utawala wa kisheria,itisha uchaguzi na kujiuzulu kama mkuu wa majeshi.Rais Jemadari Musharraf alitangaza amri ya hali ya hatari siku ya Jumamosi,kufuatia machafuko ya miezi kadhaa nchini humo.