1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WASHINGTON: Rais George W: Bush wa Marekani azindua mkakati mpya wa serikali yake nchini Iraq.

11 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCbr

Rais wa Marekani, George W. Bush, amezindua mkakati mpya wa serikali yake nchini Iraq.

Rais George Bush alilihutubia taifa lake kwa njia ya televisheni ambapo alisema mpango wake utajumuisha kupelekwa wanajeshi zaidi ya elfu ishirini wa ziada nchini Iraq.

Wengi wa wanajeshi hao watapelekwa kusaidia vikosi vya Iraq kuhakikisha usalama mjini Baghdad.

Wanajeshi wengine watapelekwa katika jimbo la Anbar linalokabiliwa na mzozo.

Kwa mara ya kwanza, Rais George Bush, amekiri kwamba sera za serikali yake nchini Iraq hazijafanikiwa kufikia sasa.

Rais Bush amesema

"Wanajeshi wetu wamepigana kwa ukakamavu nchini Iraq. Wametekeleza yote tuliyowataka kutekeleza. Endapo makosa yametendeka basi lawama ni kwangu mimi. Ni dhahiri shahiri kwamba tunahitaji kubadilisha mikakati yetu nchini Iraq"

Rais George Bush amesema mwelekeo wake mpya nchini Iraq hautaleta ufanisi wa mara moja na wakati huo huo akavitahadharisha vikosi vya Marekani kwamba mwaka huu huenda mambo yakazidi kutatizika nchini Iraq.

Viongozi wa Chama cha Democratic katika bunge wamemshutumu Rais Bush kwa mpango wake wa kuongeza idadi ya wanajeshi nchini Iraq wakisema kuwa hatua hiyo itazidisha vurugu.